Ikiwa ni miaka miwili sasa ya filamu ya Royal Tour leo Mei 2, 2024 Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi ameshiriki mahojiano maalum kupitia kipindi cha JANA na LEO kinachoruka kupitia Radio ya Wasafi Fm “live” kutoka katika Geti la Marangu, Mlima Kilimanjaro.
Geti hilo ni mojawapo ya maeneo alikofika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifanya filamu ya “Tanzania: The Royal Tour.
Dkt. Abbasi ametumia wasaa huo kuelezea mafanikio ya Filamu ya Royal Tour katika Mlima Kilimanjaro ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24 Makadirio ya wageni ilikuwa ni 48,618 lakini hadi kufika Aprili 30, 2024 Hifadhi ya KINAPA imepokea wageni 53,739.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24 makadirio ya mapato yalikuwa Bilioni 78 hata hivyo hadi kufikia Aprili 30, 2024 mapato yameongezeka na kuwa zaidi ya Bilioni 84.
Hivyo inaonesha kuwa filamu ya Royal Tour imelipa na inazidi kuinufaisha Tanzania.