Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Mei 2
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameendelea kufungua milango kwa wahisani na wadau wa maendeleo kupitia Sekta binafsi ili kumuunga mkono jitihada za Serikali kutoa huduma kwa watanzania.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mzava, alieleza hayo wakati Mei 2, 2024 alipokuwa halmashauri ya Mji Kibaha, kuzindua mradi wa kisima kirefu cha maji shule ya msingi Visiga, mradi ambao umegharimu milioni 16.870 kutoka kwa mfadhili Taasisi ya REHEMA FRIENDSHIP AND SOLIDARITY TRUST na jengo la ukumbi wa destiny ,mradi wa mdau wa maendeleo ambao umegharimu Milioni 500.
“Ndio maana tunaona matunda yake Leo tunashuhudia wenzetu Rehema Foundation wameweza kuunga mkono na halmashauri pamoja na wilaya mmekuwa tayari kuwapa ushirikiano kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa “alisema Mzava.
Mzava alitoa wito wahisani na wafadhili mbalimbali kuendelea kukaribishwa maana milango ipo wazi kwani Serikali yetu imeshafungua mlango ” alisisitiza Mzava.
Vilevile, alieleza Serikali, wahisani, wadau wanapotoa fedha za miradi wanapenda kuona inalindwa na kutunzwa ili idumu kwa kipindi kirefu.
Hata hivyo,Mzava alizitaka taasisi wezeshi za Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wanaotaka kuwekeza .
Aliomba jamii itunze na kulinda miradi mbalimbali iliyopo kwenye maeneo yao.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mwalimu Mkuu Shule ya msingi Visiga, Mwalimu Ali Seif Ali alisema, ulianza 6,juni 2023 na kumaliza juni 26 ,2023 .
Alieleza, kisima kinafaida kubwa ni mkombozi mkubwa kwa wanafunzi na walimu pamoja na jamii inayozunguka shule kwa kupunguza changamoto ya maji.
Ali alisema, shule ina idadi ya wanafunzi takriban 1,265 kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba na kabla ya mradi huo ,shule ilikuwa inatumia gharama kubwa kulipa bili ya maji kwenda DAWASA ambapo shule ilikuwa inalipa zaidi ya 285,000 kwa mwezi.
Nae mkurugenzi wa kampuni ya Destiny Veronica Joseph alieleza , mradi wa ukumbi utasaidia kuongeza uchumi ,na kulipia kodi ya Serikali na kutoa fursa za ajira.