KUPANUA ENEO LA UWAGILIAJI
Katika mwaka 2022/2023 na mwaka 2023/2024 Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya umwagiliaji yenye jumla ya hekta 256,185.46. Kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hiyo kutaongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 727,280.6 mwaka 2020/2021 hadi hekta 983,466.06 ambazo ni sawa na asilimia 81.95 ya lengo la hekta 1,200,000 ifikapo mwaka 2025.
UTEKELEZAJI WA MWAKA 2023/24
Mwaka 2023/24, Tume imejitahidi kutekeleza miradi ya kilimo cha umwagiliaji kwa kutenga jumla ya Shilingi Bilioni 361.5. Hadi Aprili 2024, miradi 231 kati ya 780 imeendelea kutekelezwa, ikihusisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu mpya, ukarabati wa skimu za zamani, na ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji. Pia, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umefanyika katika mabonde na skimu za umwagiliaji.
MPANGO WA MWAKA 2024/25
Katika mwaka ujao wa 2024/25, Tume inakusudia kuendelea na miradi ya umwagiliaji iliyopangwa awali, ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi ya ujenzi na ukarabati. Miradi mipya itajumuisha ujenzi wa skimu mpya, ukarabati wa skimu za zamani, na upembuzi yakinifu na usanifu wa mabwawa na skimu mpya.
KUHAKIKISHA MIUNDOMBINU ENDELEVU
Tume ina mpango wa kutoa mafunzo kwa wakulima viongozi 10,000 katika skimu 1,230 kuhusu uendeshaji na matunzo ya miundombinu ya umwagiliaji na ukusanyaji wa ada. Pia, Tume itasajili vyama vipya vya umwagiliaji 500 na kusimamia vyama vilivyosajiliwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa NIRC-iMIS na POS.
Kupitia Bunge la Bajeti linalondelea Bungeni Dodoma,Bunge linatarajiwa kujadili na kabla ya kupitisha Jumla ya Shilingi Bilioni 393.3 zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza mipango ya maendeleo kwa mwaka 2024/2025, huku Tume ikiendelea na juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo cha umwagiliaji nchini.