Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akisisitiza jambo kwa wananchi wa Kibada, Wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua athari za miundombinu ya barabara na madaraja zilizotokana na mvua za El-Nino katika barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji (km 41).
Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi John Mkumbo akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, pamoja na viongozi wengine wakati wakikagua miundombinu ya barabara na madaraja katika barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji iliyoathiriwa na mvua za El Nino, Mkoani Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akikagua barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji (km 41) ambayo imeathiriwa na mvua zilizonyesha za El Nino Wilayani Kigamboni Mkoani Dar es Salaam.
Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi John Mkumbo akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, wakati wakikagua miundombinu ya barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji (km 41), iliyoathiriwa na mvua Mkoani Dar es Salaam.
Muonekano wa juu wa sehemu ya barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji (km 41) ambayo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameikagua Wilayani Kigamboni katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua Mkoani Dar es Salaam.
……………………
Serikali yatoa ahadi kufanya kila linalowezekana barabara zipitike, mvua zikiisha ujenzi utaanza rasmi
Waziri wa Ujenzi Mhe Innocent Bashungwa akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila na wataalam wengine leo April 29, 2024 amefanya ziara katika maeneo yaliyoathirika na mvua katika Wilaya ya Kigamboni na baadae kukagua eneo la Kivuko Magogoni
Mhe Waziri alianza ziara yake katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo alipatiwa taarifa fupi ya athari ya mvua katika Mkoa huo kutoka kwa mwenyeji wake Mh Albert Chalamila na Meneja wa TANROAD mkoa huo.
Akiwa katika barabara ya kibada-mwasonga Waziri Bashungwa amekagua barabara hiyo ambayo imeharibiwa na mvua ambapo ametoa kauli ya Serikali kuwa tayari mkandarasi ameshapatikana barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami urefu wa Km 51 “wananchi wawe na subra Serikali kwa sasa inafanya ukarabati wa kawaida kurejesha mawasiliano lakini mvua zikiisha tu ujenzi utaanza rasmi” Alisema Waziri Bashungwa
Aidha akiwa katika barabara ya Kigamboni-mwasonga eneo la Magogoni alipata wasaa wa kukagua barabara hiyo na kuongea na wananchi ambapo amewahakikishia kuwa kutakuwa na timu maalum ya kufanya tathimini ya uharibifu wa miundombinu katika Mkoa huu ambayo itaripoti katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ikimaliza tathimini yake maeneo yote yenye changamoto yatapatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila amesema ukichunguza kwa umakini maeneo yenye mafuriko utaona nyumba zimejengwa katika mikondo ya maji hivyo kuzuia maji kupita ambapo amewataka wataalam kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo ambayo njia za asili za maji zimezibwa ili ikilazimu kama kuna Kuta zibomolewe.
Vile vile Waziri Bashungwa amekagua Kivuko eneo la Magogoni kujionea Changamoto za kivuko hicho na kesho anatarajia kuendelea na ziara yake ikiwa ni siku ya pili katika Mkoa huo.