Mwili wa marehemu Noel Mwingira ukipelekwa eneo ulipohifadhiwa kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Furaha Tv na Furaha Fm Bw. Furaha Dominic akizungumza waandishi wa habari wakati wa kuaga mwili wamarehemu Noel Mwingira katika viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar es Salaam.
………………………
Vijana nchini wametakiwa kuwa na upendo, umoja na mshikamano katika maisha yao hapa duniani jambo ambalo litasaidia kupata fursa za maendeleo pamoja na kuepuka majivuno.
Akizungumza leo Aprili 29,2024 katika viwanja vya Leaders Kinondoni, jijini Dar es Salaam wakati wa shughuli za kuaga mwili wa aliyekuwa mpiga picha wa Ayo Tv Noel Mwingira, Mkurugenzi wa Furaha Tv na Furaha Fm Bw. Furaha Dominic, amesema kuwa msiba wa Noel unatukumbusha tuishi maisha yanayotupendeza sote na kuacha tabia ya kuumizana.
Bw. Dominic amesema kuwa marehemu amekuwa akiishi maisha ya kujitoa kwa wezake pamoja na kuonesha ushirikiano kwa kila mtu.
“Tuungane kwa pamoja kumuombea Noel, kifo chake iwe fundisho ili na sisi tuwe na kesho njema, tupendane na tupeane fursa katika maisha yetu hapa duniani” amesema Bw. Dominic.
Amesema kuwa Noel alikuwa kijana mpambanaji asiyekuwa na makuu katika maisha yake hivyo kupitia kifo chake vijana wanapaswa kupendana na kuiga maisha yake ambayo yameacha alama hapa duniani.
“Ukiona kijana mwezako amepata matatizo tuungane kwa pamoja kumsaidia, huku tukiendelea kufanya kazi kwa bidii” amesema Bw. Dominic.
Amesema kuwa kifo chake kinaumiza watu wengi na kimeacha majonzi, lakini ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu hatuna budi zaidi ya kuyakubali.
“Ametuachia funzo kuwa muda, saa na dakika yoyote linaweza kutukuta lolote, ni namna gani unaondoka na unaacha alama gani ambapo wezako wanaweza kukukumbusha” amesema Bw. Dominic.
Noel Mwingira alifariki kwa ajali ya Pikipiki maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na amezikwa leo katika Makaburi ya kinondoni.
Picha mbalimbali zikionesha waombolezaji mbalimbali wakishiriki katika mazishi ya marehemu Noel Mwingira katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es salaam.