Na Mwandishi wetu, NCAA.
Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imepongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Jengo la makao makuu wa NCAA linalojengwa Karatu Mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NCAA Jenerali Venance Mabeyo (mstaafu) amesema ujenzi wa jengo hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kupunguza shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ili kuboresha maisha ya wananchi.
“Mtakumbuka Serikali ilielekeza kupunguza shughuli za binadamu ndani ya Hifadhi, tayari zaidi kaya 1300 zenye watu zaidi ya 8300 zilishahama ndani ya Hifadhi, Menejimenti ya NCAA nayo iliamua kuhamisha makao yake makuu kwa kujenga ofisi nje ya Hifadhi na tumeona ujenzi unakwenda vizuri na kwa ubora unaotakiwa” alisema Jenerali Mabeyo.
Jenerali Mabeyo ameielekeza Menejimenti ya NCAA kuendelea kumsimamia mkandarasi anayejenga jengo hilo ili likamilike kwa wakati na kuzingatia viwango kadri ya mkataba wa ujenzi ulivyosainiwa.
Kaimu kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Victoria Shayo ameieleza bodi hiyo kuwa ujenzi wa jengo hilo umeenda sambamba na zoezi la upandaji miti katika eneo lote la mradi ili kuimarisha uoto wa asili na kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kutunza mazingira kupitia upandaji miti.
Kwa upande wake Kamishna msaidizi mwandamizi, Huduma za uhandisi NCAA Eng. Daniel Chegere amesema kuwa mradi wa ujenzi wa ofisi hizo unaenda sambamba na ujenzi wa Nyumba 3 za makazi ya Viongozi wa NCAA ambapo ujenzi umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi Juni, 2024.
Kukamilika kwa jengo hilo kutatoa fursa kwa watumishi wa mamlaka hiyo kuwa na ofisi za kudumu tangu walipohama kutoka ndani ya hifadhi mwaka 2021.