Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,wakisubiri huduma ya uchunguzi na matibabu  kutoka kwa Madaktari Bingwa wa mikoa ya Songwe,Mbeya na Ruvuma waliopo kwenye kambi maalum  kwa ajili ya kutoa huduma za Kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Songea(Homso).


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,akisalimiana na  Madaktari Bingwa wa mikoa ya Ruvuma,Songwe na Mbeya  baada ya kufungua  zoezi la uchunguzi na matibabu ya Kibingwa kwa wananchi wa mkoa Ruvuma yanayoendelea katika Hospitali ya Mkoa mjini Songea.


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,akizungumza  na wananchi,watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa Songea(Homso) na Madaktari Bingwa kutoka mikoa ya Songwe,Mbeya na Ruvuma kabla ya kuanza kwa utoaji wa huduma za Kibingwa zinazoendelea kutolewa katika Hospitali hiyo.

………….

Na Mwandishi wetu, Songea

TIMU ya madaktari Bingwa kutoka mikoa ya Ruvuma,Songwe na Mbeya wameanza kutoa huduma za  uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa Songea(Homso)Dkt Majura Magafu amesema,uchunguzi na matibabu  hayo yatahusisha magonjwa ya akina Mama,magonjwa ya ndani kama vile shinikizo la damu,kisukari na figo.

Majura ameyataja magonjwa mengine yatakayochunguzwa ni magonjwa ya watoto,mifupa,upasuaji,macho,kinywa,meno,upasuaji wa midomo sungura,masikio,pua,koo,afya ya akili,ngozi,moyo,mfumo wa chakula na saratani.

Amesema,wizara ya afya na Tamisemi inaendelea kuboresha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kuwatumia madaktari waliopo katika Hospitali za rufaa za mikoa,kanda,taasisi na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kwa mujibu wa Dkt Majura,lengo kuu la kuwatumia madaktari bingwa waliopo katika Hospitali na taasisi zetu ni kufikisha matibabu ya kibingwa  kwa wananchi wengi na kwa wakati  ili zisaidie wanannchi kupata hudum bora na kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Ahmed Abbas,ameipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi kwa  ajili ya kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika mkoa wa Ruvuma.

Amewataka Madaktari Bingwa,kutowasubiri wananchi(wagonjwa)hadi wafike  Hospitali badala yake, wahakikishe wanajikita zaidi katika kutoa elimu inayohusiana na madhara,namna ya kujikinga na pia kuwafuata wananchi waliko  jambo litakalowezesha  kuwafikia watu wengi.

Alisema,serikali itaendelea kuwekeza kwa kutoa fedha na kuajiri wataalam kwa ajili ya kuboresha huduma za  afya kwa wananchi na amewahakikishia wananchi kwamba,katika kipindi chote za kambi  hiyo watapata huduma bora.

Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge,ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa  za kambi hiyo kwani zinatoa unafuu na kupata huduma za kibingwa kwa gharama nafuu na kupunguza usumbufu wa kufuata huduma mbali na maeneo yao.

Awali Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Lous Chomboko alisema,kambi ya Madaktari bingwa katika mkoa wa Ruvuma itakuwa ya   siku tano  kuanzia leo tarehe 29 hadi tarehe 4 mwezi Mei.