…………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Mwanza taasisi hiyo inachunguza miradi saba ya maendeleo inayogharimu sh.bilioni 6.1 kati ya 15 yenye thamani ya sh.bilioni 19.11.
Pia, ilichambua mfumo wa mapato ya kodi ya zuio na kuleta matokeo chanya na kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoani humu kukusanya sh. milioni 68.1 za kodi hiyo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,James Ruge,amesema leo alipozungumza na waandishi wa habari kuwa wanaendelea na uchunguzi katika miradi saba ya maendeleo inayotekelezwa kwa gharama ya sh.6,100,276,762.79 kati ya miradi 15 inayogharimu sh. 19,110,131,068.79.
Amesema miradi hiyo ni ya sekta za afya, elimu, maji, uchukuzi na utawala,iliyofuatiliwa na kukaguliwa katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu, ililenga kufahamu ubora na thamani ya fedha zilizotumika.
“Miradi hiyo 15 ya maendeleo iliyokaguliwa saba, ilikutwa na mapungufu ya kutokamilika kwa wakati (nje ya muda wa mkataba),ukiwemo wa jengo la utawala la Halmashauri ya Kwimba mkataba umevunjwa,ukarabati wa lambo la maji ya kunyeshwa mifugo Nymbiti vifaa vya ujenzi kuharibika sababu ya utunzaji mbovu na vingine viliibwa,”amesema Ruge.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TAKUKURU, majalada ya uchunguzi yamefunguliwa na unaendelea kwa miradi saba iliyobainika kuwa na mapungufu makubwa katika sekta ya maji mitatu huku sekta za elimu,uchukuzi,afya,mifugo na utawala zenye mradi mmoja mmoja nazo zikichunguzwa.
Ruge amesema taasisi hiyo ilichambua mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya kodi ya zuio katika Halmashauri ya Manispaa Ilemela na kuiwezesha TRA mkoani humu kukusanya sh.68,164,545.
Pia kazi hiyo ya uchambuzi wa mfumo wa mapato ya kodi ya zuio imesaidia kutambuliwa kwa taasisi 37 katika wilaya ya Kwimba,11 kati ya hizo zimesajiliwa na kupewa namba ya mlipa kodi (TIN),ili zilipe kodi hiyo kwa mujibu wa sheria.
Ruge amesema mafanikio hayo yametokana na maazimio yaliyowekwa na TAKUKURU ya namna bora ya kukusanya kodi ya zuio baada ya uchambuzi wa mfumo kufanyika ambapo mapungufu mbalimbali yalibainika ikiwemo halmashauri kutokusanya kodi hiyo,uelewa mdogo wa kodi ya zuio kwa wafanyabiashara na watoa huduma baadhi hasa mafundi ujenzi (local) kutokuwa na TIN.
“Moja ya majukumu ya TAKUKURU kudhibiti mianya ya rushwa kwa kuchambua mifumo ya utendaji kazi katika taasisi za umma na zisizo za kiserikali,ili kubaini mianya hiyo ya rushwa na hatimaye kushauri namna bora kutoa huduma na kuepuka vitendo vya rushwa,”amesema.
Ruge ameeleza kuwa katika kipindi hicho cha Januari hadi Mwachi, 2024 ,kwa kazi za uchunguzi walipokea taarifa 70 kati ya hizo 44 za vitendo vya rushwa na 26 hazikuhusiana na vitendo hivyo na uchunguzi uko hatua mbalimbali.
Ameongeza kuwa,taarifa 18 wahusika walishauriwa,tano zilifungwa, moja ilihamishiwa idara nyingine na mbili zinafuatiliwa huku upande wa mashitaka,mashauri yaliyokuwa mahakamani, jamhuri ilishinda kesi tano kati ya 33 ambapo kesi 28 zingali zinaendelea kusikilizwa .
Aidha, katika kipindi hicho makundi mbalimbali ya wananchi yalielimishwa madhara na makosa ya rushwa pamoja na wajibu wao wa kushiriki kuzuia na kupambana na rushwa ambapo semina 71 zilifanyika kwa watumishi wa sekta za umma na binafsi.