Na Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameagiza Polisi kufanya msako na kuwakamata watu watatu wa familia moja wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la mauaji ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Kampimbi kata ya Ndungu, Charles Johnson Mkuruto(58).
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, mnamo Aprili 26 mwaka huu majira ya saa tano na nusu asubuhi huko kitongoji cha Kampimbi kijiji cha Ndungu kata ya Ndungu mtu mmoja aitwae Johnson Mkuruto(58) Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sinangoa ‘A’ aliuwawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya kichwani na nyuma ya bega la kulia.
Alisema kuwa, Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Ardhi kata ya Ndungu alikatwa na watu watatu ambao aliwataja kwa majina kuwa ni Mohamad Makundi, Hamad Makundi na Mnandi Makundi na kutoweka kusikojulikana.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, sababu ya mauaji hayo ni mgogoro wa Ardhi uliopo Mahakama ya Ardhi ya Ndungu.
“Baraza la Ardhi jana lilienda eneo la mashamba yanayobishaniwa ndipo watuhumiwa walimvamia marehemu na kumkatakata na kitu chenye ncha kali kisha kukimbia” Alisema Kasilda.