Na. John I. BERA – ARUSHA
Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuonesha ubabe wake kwenye mbio ambapo kwa upande wa wanaume imeibuka mshindi wa tatu kwenye mbio za mita 3000 na mbio za 1500, mshindi wa tatu kwenye mbio za mita 800 huku ikimaliza mshindi wa tatu kweny mbio za mita 200 katika Mashindano
Mei Mosi 2024 yanayoendelea kufanyika Jijini Arusha.
Akizungumza mara baada ya ushindi huo Bw. Elibariki Buko ambaye ndiye mshindi namba tatu wa mita 3000 na 1500 amesema, ushindi huo ni matokeo ya uongozi makini wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuhakikisha inahamasisha michezo ili kutangaza Utalii
” Ushindi huu sio wa kwangu mimi bali ni ushindi wa Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wamekuwa msaada mkubwa kwetu kuanzia maandalizi hadi hatua hii. Niwashukuru sana Mimi pamoja na watumishi wenzangu kwa kuendelea kutuwezesha kushiriki katika michezo hii” Amesema Buko
Ametumia fursa hiyo kuihakikishia Menejimenti ya Wizara hiyo kuwa yeye pamoja na wenzake watatumia michezo hiyo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini huku akiomba kuendelea kupewa nafasi zaidi katika kushiriki katika mashindano mengine ili waweze kukidhi ndoto na maono aliyonayo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya utalii kitaifa na kimataifa.
‘’Tumeanza kutangaza utalii na vivutio vya utalii vilivyopo hapa Arusha na hata vivutio vingine ambavyo haviko hapa kama Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambayo iko kusini mwa Tanzania .” amesema Buko.
Ameongeza,’’ imetusaidia pia kujenga ushirikiano na afya kwani nina uhakika mara tukaporudi katika maeneo yetu ya kazi umakini na uhodari katika kuhudumia watanzania utaongezeka’’
Kwa upande wake Athumani Simbiri ambaye ndio mshindi wa tatu kwenye mbio za mita mita 200 kwa wanaume amesema, aliamini atashinda mbio hizo mara baada ya kufanya maandalizi ya kutosha huku akiwapongeza Walimu kwa kuwaandaa vizuri kwa ajili na shindano huo
‘’Tulijiandaa vizuri, haikuwa rahisi lakini nawashukuru sana Walimu wetu walifanya kazi nzuri ya kutuandaa kwa ajili mchezo huu’’ Alisema
Naye mshindi wa mbio za mita 800, Kispan Saing’ati amesema, lengo lao ilikuwa kufanya vizuri na kupeperusha bendera ya Wizara, na sasa wamefurahi kuona wameweza kutangaza Utalii kupitia ushindi huo.
Aidha, Baada ya ushindi huo leo, Wizara ya Maliasili na Utalii hadi sasa imefanikiwa kuchukua jumla ya Vikombe 6 ikiwemo vikombe 4 kwa upande wa riadha, 1 kwa upande wa drafti pamoja na kikombe 1 kwa Upande wa Tufe.
Vilevile imefanikiwa kuingia nusu fainali ambapo hapo kesho Mei 27, 2024 itamenyana vikali na Timu ya Mahakama ambapo mshindi ataingia fainali ya mchezo huo.