Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, akizungumza wakati akifunga mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Natu El Maamry Mwamba, uliofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar Es Salaam.
Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Fedha, ambaye pia ni Afisa Utumishi wa wizara ya hiyo Bw. Tumwesige Kazaura, akiwasilisha hoja mbalimbali kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Bi, Jenifa Omolo (hayupo pichani), katika mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi mwaka 2023/2024 uliyofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar Es Salaam.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Leonard Mkude, akifuatilia mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi mwaka 2023/2024 uliyofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar Es Salaam ambapo mkutano huo umehudhuriwa na Watumishi wa Wizara ya Fedha kutoka maeneo mbali mbali kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji kwa ajili ya ustawi wa wizara hiyo.
Mmoja wa wajumbe waliyohudhuria Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Fedha Bi. Mariam Kiange ambaye pia ni katibu wa wanawake Wizara ya Fedha, akichangia hoja wakati wa majadiliano katika mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi mwaka 2023/2023, uliyofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar Es Salaam.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha kutoka mikoa mbalimbali wakifuatilia hoja zilizokuwa zikijadiliwa katika mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi mwaka 2023/2024, uliofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar Es Salaam.
…………………….
Na Asia Singano – WF, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Omolo amewataka watumishi wa Umma kutimiza majukumu yao kwa wakati na weledi na kuwekeza kwa ajili ya Maisha ya uzeeni ili kuepuka usumbufu katika kipindi cha kustaafu.
Bi. Omolo ametoa wito huo wakati wa mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Fedha mwaka 2023/2024, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, katika ukumbi wa Kilimanjaro, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar Es Salaam.
‘’Ni vyema ukamaliza majukumu yako kwa wakati husika ili angalau miezi miwili kabla ya kustaafu kila kitu chako kiwe sawa siyo mpaka siku chache kuelekea kustaafu bado una majukumu mengi hujayakamilisha”, alisema Bi. Omolo.
Alisisitiza kuwa ni vyema watumishi wakawekeza wakati wakiwa kazini ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na uwezo wa kuendesha maisha na kukidhi mahitaji yao muhimu baada ya kustaafu.
‘’Mada ya uwekezaji ni muhimu sana kama ilivyowasilishwa wafikishieni watumishi wote umuhimu wa kuwekeza, tunaweza kuwekeza UTT AMIS, NIC na Benki lengo ni kuhakikisha kuwa tunavyofanya kazi tuwe na namna ya kuwekeza kwa ajili ya familia zetu na kujiandaa kustaafu’’, alisisitiza Bi. Omolo
Aliongeza kuwa Uongozi wa Wizara hiyo utahakikisha kuwa unatatua changamoto mbalimbali zinazoweza kukwamisha utendaji wa watumishi na kuhakikisha wanapata stahiki.
Aidha Bi Omolo amewataka watumishi hao kushiriki kikamilifu katika kutekeleza bajeti iliyopitishwa kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali za kuleta maendeleo ya nchi.
Mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya fedha hufanyika kila mwaka ambapo hutoa fursa kwa watumishi kujadili na kuwasilisha changamoto mbali mbali katika maeneo ya kazi ili ziweze kutatuliwa.