Viongozi wa idara ya uhamiaji kutoka mkoani Arusha na jijini Dar es Salaam wakisikiliza maoni kutoka kwa washiriki wa mkutano wa idara ya uhamiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji mkoa wa Arusha uliofanyika jijini Arusha leo.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakisikiliza maoni mbalimbali .
…………………….
Happy Lazaro,Arusha.
Jumla ya wahamiaji haramu 425 wamekamatwa na idara ya uhamiaji mkoa wa Arusha katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia januari hadi desemba mwaka huu.
Akiongea kwenye mkutano wa idara ya uhamiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji mkoa wa Arusha ,Mkuu wa uhamiaji mkoa wa Arusha
,Abdallah Towo amesema kuwa,wahamiaji hao haramu wamekamatwa kutoka nchi mbalimbali na Kati yao 69 wamefikishwa mahakamani ,huku 66 wakifukuzwa nchini na wengine 17 wakifungwa.
Amesema kuwa,ofisi ya uhamiaji mkoa wa Arusha imeitisha mkutano wa wadau wa huduma za uhamiaji kwa lengo la kupokea maoni na kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu changamoto mbalimbali za kiuhamiaji mkoani hapa.
Towo amefafanua kuwa,katika kipindi cha Januari 2019 hadi novemba idara ya uhamiaji imepokea pasipoti za kieletroniki 6,231 na shahada za dharura za kusafiria 29,472 kwa watanzania waliohitaji kusafiri nje ya nchi.
Aidha katika sekta ya utalii kwa kipindi hicho idara ya uhamiaji mkoa wa Arusha imetoa Viza na pasipoti 1,402 kwa wageni walioingia nchini kwa madhumuni mbalimbali ya utalii.
Amesema kuwa,katika mpaka wa Namanga Raia wa Tanzania na wageni kutoka nchi mbalimbali wapatao 124,106 wamewezeshwa kuingia nchini na ambapo Raia na wageni 125,681 wamewezeshwa kutoka nchini.
Amesema kuwa,kwa upande wa wawekezaji idara hiyo imetoa jumla ya vibali vya ukazi 517 kwa wageni waliiongia nchini kwa madhumuni ya kuwekeza katika sekta ya madini ,viwanda na biashara.
“katika kuhakikisha kuwa mkoa wa Arusha upo salama idara ya uhamiaji imeimarisha udhibiti wa wahamiaji haramu kwa kufanya kazi misako na Doria kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huu na kwa kufanya hivi tumeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa Sana.”amesema Towo.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo Mkuu wa wilaya ya Karatu,Theresia Muhongo amewataka watendaji wa idara ya uhamiaji kuzingatia maadili na miongozo iliyopo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi ili kuweza kutatua changamoto zinazokabiliwa na idara hiyo.
Naye Afisa uhamiaji mkoa wa Kilimanjaro,Tunu Ng’ondya amesema kuwa, changamoto ya wahamiaji haramu iliyopo katika maeneo mbalimbali zinafanana ambapo kwa mkoa wa Kilimanjaro wahamiaji haramu wamekuwa wakitoka Ethiopia kwenda nchi za kusini.
Amesema kuwa,wamekuwa wakishirikiana kwa pamoja na vikundi vya ulinzi na usalama chini ya uongozi wao katika kuhakikisha kuwa mkoa huo unakuwa salama,huku wakishirikiana na maafisa watendaji wa kata ambao wamekuwa makini kutoa taarifa kwenye vyombo husika pindi wanapoona wageni katika maeneo yao.