Na Sophia Kingimali.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Profesa Adolf Mkenda ametoa rai kwa walimu wakuu nchini kupokea watoto wanaopelekwa kwenye shule zao wanaotoka kwenye majanga ya mafuriko ili kuendelea na masomo huku taratibu zingine zikiwa zinaendelea.
Hayo amezungumza leo Aprili 24,2024 jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyeesha na kupelekea miundombinu ya shule kuharibika hivyo imepeleka baadhi ya shule kufungwa na baadhi ya wakazi kuhama na kwenda sehemu nyingine zenye usalama.
Amesema watoto waliotoka kwenye shule zenye changamoto wanapaswa kupokelewa na kuendelea na masomo wakati afisa elimu kata akiendelea na taratibu nyingine.
“Ikiwa shule zimefungwa kutokana na uharibufu wa miundombinu lakini pia familia zimehama kutokana na mafuriko basi kule wanapoenda watoto wapokelewe na waendelee na masomo mpaka pale taratibu za ukarabati zitakapokamilika”,Amesema Profesa Mkenda.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa wazazi pindi wanapoona mvua kubwa kutowaruhusu watoto kwenda shule lakini pia walimu wakuu wanapaswa kuchukua hatua za haraka pindi wanapoona hali mbali ya hewa kwa kuwaruhusu mapema shule na kusimamisha masomo kwa muda huku wakiangalia namna ya kuweza kufidia siku hizo ambazo watakua wamesimamisha masomo.
“Kamishna wa elimu atatoa muongozo na kuruhusu mabadiliko katika kalenda ya ufundishaji ili kusaidia kwenye swala la mvua watoto wasiumie”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa serikali kupitia wizara itashirikiana na wazazi ambao watoto wao wanasoma katika shule binafsi ambazo zimefungwa kutokana na uharibifu wa miundombinu kupata shule watakazozichagua na kwa maelewano yao ili kuwapeleka watoto kuendelea na masoma.
Hata hivyo amezipongeza shule binafsi ambazo ziliamua kusitisha masomo kwa muda katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyeesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha Profesa Mkenda ametoa onyo kwa madereva wa magari ya shule kutopitisha magari hayo sehemu hatarishi ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea.
“Kutu cha kwanza katika shule zetu ni usalama wa watoto wetu na wafanyakazi katika taasisi zetu hivyo niwaonye madereva wakiona dalili zozote za hatar waache wasije wakaingiza watoto wetu kwenye hatari.”Amesema.
Aidha amesema serikali kupitia wizara unaendelea kufuatili miundombinu iliyoharibika na kufuatilia kwa karibu za hali ya hewa ili waweze kurejesha miundombinu hiyo huku shule ambazo zimebomoka kutokana na kuwa kwenye maeneo hatarishi mabondeni wataangalia sehemu salama na kuzijenga upya.