Na. Zillipa Joseph, Katavi.
Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa kushirikiana na Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi imefanya mawasiliano na kampuni ya simu ya Tigo na kufanikiwa kuwezesha malipo ya kijiji cha Ibindi kufuatia kuwepo kwa mnara wa mawasiliano katika kijiji hicho.
Kwa mujibu wa Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Katavi Faustine Maijo kijiji hicho kilikuwa hakijapokea malipo tangu mwaka 2016 ambapo kila mwezi walipaswa kulipwa kiasi cha shilingi laki tatu bila VAT.
Katika hatua nyingine TAKUKURU imefuatilia utekelezaji wa miradi mitano yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 5.82; kwa kipindi cha cha miezi mitatu kuanzia Januari 2024 hadi Machi mwaka huu inayohusu sekta ya elimu na miundombinu ya barabara. |
Hayo yamebainishwa na Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Faustine Maijo wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema leo.
Maijo ameeleza kuwa katika miradi hiyo waliyofuatilia wamebaini mapungufu mbalimbali ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi.
Kuhusu malalamiko ya Rushwa amesema TAKUKURU katika kipindi hicho cha miezi mitatu wamepokea malalamiko 41 yanayohusiana na vitendo vya rushwa katika ya malalamiko hayo 38 yalikuwa ni ya rushwa na matatu hayakuwa ya rushwa .
Maijo amefafanua kuwa kutokana na taarifa hizo za malalamiko ya rushwa wameweza kufungua majalada 38 yaliyotokana na taarifa hizo ambapo uchunguzi wa majalada matatu umekamilika na katika kipindi hicho cha miezi mitatu mashauri manne yamefunguliwa mahakamani na kufanya kuwa na kesi nane zinazoendelea mahakamani.
Pia amewaonya watu wanaofanya utapeli kwa kujifanya kuwa ni maafisa wa TAKUKURU na kutoa wito kwa wananchi kuendeleza ushirikiano na kuwafichua matapeli wanaotumia vibaya jina la taasisi hiyo.