Na WAF – Dar Es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kuwekeza zaidi kwenye kinga na sio tiba ili kupunguza gharama za matibabu pamoja na kuepuka magonjwa Yasiyoambukiza ikiwemo Saratani kwa kufanya mazoezi na kuzingatia mtindo bora wa maisha.
Waziri Ummy ametoa wito huo Aprili 20, 2024 baada ya matembezi yaliyofanyika kwa ajili ya harambee za kuchangia ujenzi wa Hospitali ya kina mama ya MEWATA – ‘Well Women Center (WWC) iliyopo Mbweni Jijini Dar Es Salaam.
“Matembezi haya yanafanyika kwa ajili ya kuanzisha harambee za kuchangia ujenzi wa Hospitali ya kina mama ya MEWATA – WWC, kwakweli ni jambo la msingi kwa sababu litongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za wanawake na watoto nchini Tanzania”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2020, zinaonesha kuwa, tatizo la Saratani ya matiti na Saratani ya mlango wa kizazi nchini limekuwa likiongezeka mara kwa mara.
“Katika kila watu 100,000 watu 10 hugundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani ya matiti na watu 25 kwa kila watu 100,000 hugundulika kuwa na ugonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi, tuwahi kupima na kutibu Saratani kwa kuwa tukiweza kuzigundua mapema zinazuilika”. Amesisitiza Waziri Ummy
Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuhakikisha huduma za kinga na matibabu ya Saratani zinapatikana nchini kote kwa kuongeza vituo vya uchunguzi na matibabu ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi na matiti ili kuweza kufanya uchunguzi wa awali wa Saratani hizi kwa haraka.
Pia, Waziri Ummy amesema Serikali itawaunga mkono MEWATA kufikia wanawake wote wa mjini na vijijini katika kupata elimu na huduma za Afya ili kupunguza tatizo la Saratani ya mlango wa kizazi pamoja na Saratani ya matiti.
Aidha Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi kuwapeleka watoto wao kwenda kupata chanjo ya kuwakinga na Saratani ya mlango wa kizazi kwa kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mchinga Mhe. Salma Kikwete ambae pia ni mlezi wa MEWATA amesema Taasisi hiyo imefanya kampeni kadhaa katika Mikoa Kumi na Moja (11) hapa nchini ili kuelimisha wanawake na kuwafanyia uchunguzi wa awali wa Saratani ya matiti na Saratani ya mlango wa kizazi.
“Kampeni hizi zilisaidia sana kuonesha hali halisi ilivyo juu ya ongezeko la magonjwa haya Yasiyoambukiza ikiwemo Saratani ya mlango wa kizazi na Saratani ya matiti”. Amesema Mhe. Salma