Na Masanja Mabula ,Pemba.
KATIBA ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 18 na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1984 Kifungu 18 zimezungumzia haki ya mtu kupata habari.
Aidha katika katiba zote imeelezwa kuwa “ kila mtu anayo haki ya kutafuta , kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi”.
Pia imeweka bayana kwamba “kila mtu anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake”.
Hata hivyo pamoja na katiba kueleza hivyo , bado zipo baadhi ya sheria zinazowanyima uhuru na haki ya wananchi kutafuta na kupata habari.
Zipo baadhi ya sheria kandamizi ambazo zinakuwa ni kikwazo kwa wandishi wa habari kuweza kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kuihabarisha jamii.
Miongoni mwa sheria hizo ni sheria ambazo wandishi wa habari wanaziita sheria kandamizi ni sheria ya tume ya Utangazaji Zanzibar no 7 ya mwaka 1997 kama ilivyo fanyiwa marekebisho na sharia no 1 ya mwaka 2010.
Katika hasa kifungu ya 7 (1) (b) kinachozungumzia kudhbiti na kusimamia shughuli za utangazaji , hapa tumaona kwama kifungu hiki kimeipa Tume uwepo mkubwa wa kudhibiti maudhui au habari zinazotolewa na vyombo vya habari vya kielektroniki.
Kwa mnasaba huo , nguvu hizo ilizopewa Tume ya Utangazaji zinaweza kuathiri uhuru wa kujieleza na kutoa maoni , kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu ya 18 kinachoeleza , vyombo vya habari katika kutafuta na kusambaza habari.
Katika Majukwaa na mijadala mbali mbali ya wandishi wa habari pamoja na wadau wengine wa habari wamekuwa wakipaza sauti kuomba serikali kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria zenye vifungu kandamizi na vinavyo nyima uhuru wa habari na utekeleza wa majukumu ya wandishi wa habari.
Katika Ibara ya (18) ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya mwaka 1987 na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha (18), kinaeleza bila kuathiri sheria za nchi kila mtu yuko huru kuwa na maoni yake yoyote na kutoa mawazo yake na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi.
sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar no 7 ya mwaka 1997 kama ilivyo fanyiwa marekebisho na sheria no 1 ya mwaka 2010 katika sheria hii na kifungu cha saba 7 (1) na (b) kinachozungumzia kudhibiti na kusimamamia shughuli za utangazaji, hapa neon kudhibiti lina tafsiri pana lakini kudhibiti ni ile hali ya kusisitiza uwezo wa kuelekeza na kuzuia.
Baadhi ya wandishi wa habari waliozungumza na Makala hii walisema bado sheria ya tume ya Utangazaji ni kikwazo kinachokwamisha utendaji wa kazi ya kuihabarisha jamii kama iliyoelezwa kwenye katiba.
Miongoni mwa wandishi wa habari walioizungumzia sheria hii ni Ali Massoud Kombo ambaye alitaka vyombo vinavyohusika na utungaji wa sheria ziifanyie marekebisho ili iendane na wakati uliopo kulingana uhuru ulioelewa kwenye katiba.
Alisema katiba zote mbili zimefafanua vizuri kuhusiana na uhuru wa habari, lakini hii sheria ya Tume ya Utangazaji imekuja kuviza au kupingana na uhuru ulioelezwa kwenye katiba.
“Katiba zote mbili zimezingatia sana uhuru wa kupata na kutoa habari kwa wandishi , lakini hii sheria ya Tume ya Utangazaji imekuwa ni kikwazo katika utendajikazi wa wandishi habari tunashauri tu hii sheria ifanyie marekebisho”alisisitiza.
Naye Said Omar Said Meneja wa Redio Jamii Mkoani kwa upande wake alisema kila mmoja ameweza kupata haki yake katika nchi aliopo kwa kuzingatia mahitaji anayopaswa kuyapata nchini mwake kwani watu wote wana haki sawa bila kubaguwa rangi, Dini na Ukabila.
Aidha alisema pia wanahabari nao wanahaki ya kutekeleza majukumu yao kwa kutoa habari zinazo wahusu wananchi na serikali yao bila ya kukiuka misingi ya sheria zilizopo nchini.
Aliongeza kuwa katika sheria ya tume ya Utangazaji imepewa uwezo mkubwa kwa kutumia neno kudhibiti ambalo lina maana pana na sheria haijatoa tafsiri sahihi juu ya neno kudhibiti jambo ambalo linaendelea kuwakwaza wandishi wa habari.
Neno kudhibiti lina maana pana asana unaposema kudhibiti tafsiri yake haijawekwa bayana na wazi , hii imekuwa ni changamoto katika utendaji wa kazi wa wandishi wa habari na vyombo vya habari”alisema.
Wasimanizi wakubwa katika kudhibiti na kusimamia matangazo ni Tume ya Utangazaji ambao wamepewa nguvu na uwezo mkubwa na sheria hii ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wandishi wa habari , wanaharakati na wadau wengine wa habari kwani inaviza uhuru wa vyombo vya habari.
Katibu mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Suleman Abdulla Salim akizungumzia dhamira ya kifungu hicho alisema hakina nia ya kuvikomoa vyombo vya habari na wandishi wa habari bali kimelenga kuleta ufanisi wa udhibiti wa tasinia ya habari.
“Sheria hii lengo ni sio kunyima uhuru wa kupata na kutoa habari , kama iliyoanishwa kwenye katiba zetu, bali inahimiza wandishi wa habari kufuata misingi ya kihabari na kuepusha kutoa habari zenye kupotosha”alisisitiza.
Sheria ya tume ya Utangazaji Zanzibar no 7 ya mwaka 1997 kama ilivyo fanyiwa marekebisho na sheria no 1 ya mwaka 2010 katika sheria hii na kifungu cha saba 7 (1) na (b), inahitaji kufanyiwa marekebisho ili iweze kuendana na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 18 na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1984 Kifungu 18.