Na. Mwandishi, Jeshi la Polisi Kilimanjaro
Jeshi la Polisi Nchini,limesema linatalajia kuwa, mwenyeji wa zoezi la mafunzo ya utayari kwa vitendo (Field Training Exercise – FTX) mwaka 2024 litakalojumuisha nchi 14 wanachama wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (EAPCCO) kuanzia tarehe 13 – 18, Aprili 2024.
Akitoa tarifa hiyo leo Aprili 11,2024 Msemaji wa Jesh la Polisi Nchini naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema Zoezi hilo la pamoja linatarajiwa kufanyika katika Shule ya Polisi Tanzania – Moshi ambapo takribani Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wapatao 670 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo.
DCP Misime amebainisha kuwa Kufanyika kwa mazoezi hayo kunatokana na maazimio yaliyofikiwa na Wakuu wa Shirikisho la Polisi Ukanda wa Mashariki mwa Afrika katika mikutano yao ya kila mwaka.
Ameongeza kuwa Katika mkutano uliofanyika mwezi Oktoba, 2021 Kinshasa nchini Kongo, Wakuu hao wa Polisi walipitisha azimio la zoezi hili kufanyika hapa nchini.
Pia amezitaja Nchi zinazotarajiwa kushiriki ni pamoja na mwenyeji Tanzania, Burundi, Eritrea, Djibouti, DRC Kongo, Kenya, Komoro, Ethiopia, Shelisheli, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudani Kusini na Uganda.
Msemaji wa Jeshi hilo amebainisha kuwa Lengo la zoezi hilo na mazoezi mengine yaliyopita ni kuwajengea Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali uwezo wa kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu unaovuka mipaka kama vile ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, Biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na kubadilishana uzoefu na taarifa za kitelejensia.