Na. Catherine Sungura,Pwani
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imezidi kuimarisha mtandao wa barabara ndani ya mkoa wa Pwani na kufungua uchumi wake na wananchi kwa ujumla.
Mkoa wa Pwani una mtandao wa barabara jumla ya Km 5,140 kati ya hizo Km 95 ni za lami, Km 1,100 za changarawe na Km 3,945 ni udongo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuimarisha miundombinu ya barabara za Wilaya nchini.
Mhandisi Runji amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya TARURA mkoa wa Pwani kutoka shilingi Bilioni 11 mpaka kufikia shilingi Bilioni 32 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa barabara kwa mwaka.
“Tumeongeza mtandao wa barabara za lami kutoka Km 56 hadi kufikia zaidi ya Km 97, huu ni mkoa ambao umejielekeza zaidi kwenye shughuli za viwanda kama sehemu ya uchumi na eneo mojawapo ambalo limenufaika ni barabara ya Visiga- Zegereni ambapo zaidi ya Km 12.5 za barabara zimeshakamilika”.
Amesema pia wana miji kama Mafia, Ikwiriri, Kibiti ambapo hawakuwa na mtandao wa lami kabisa na sasa Serikali imejenga.
“Tumejenga Km 2 upande wa Mafia, Km 1.6 upande wa Kibiti na Km zaidi ya 15 katika Mji wa Kibaha”, amebainisha.
Upande wa bagamoyo amesema ni mji mkongwe hivyo barabara nyingi zinahitaji matengenezo kila mwaka kuna zaidi ya Km 1 ambazo wanazifanyia matengenezo ili kuzirudisha kuwa katika hali nzuri.
“Lakini pia tunashuhudia ujenzi wa madaraja makubwa katika mkoa wetu wa Pwani, tuna daraja la Mbuchi ambalo ni zaidi ya mita 61 limekamilika, daraja la Mbwera linatumika lina zaidi ya mita 43 na pia tunatarajia kuanza kujenga daraja la Bibititi Mohamed (Mohoro) lenye urefu wa zaidi ya mita 80”.
Amesema Daraja la Mbwera limeweza kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji ambapo wananchi wanaotoka Mbwera walikuwa wanaenda kuungana na wenzao wa Muhoro ili kuunganisha na barabara kuu iendayo Mtwara kwa zaidi ya Shilingi 30,000 lakini sasa hivi wanatumia kati ya 10,000 hadi 15,000 haya ni mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya sita kwani barabara nyingi zimefungua maeneo mbalimbali katika mkoa wa Pwani.
Naye, Bi. Sofia Tebe Mjumbe wa Mtaa Zogoare amesema tangu ahamie mkoani hapo mwaka 1981 walikuwa na shida sana hususan barabara kwani barabara zilikuwa hazipitiki na wajawazito walikuwa wakipata shida kufika hosoitalini na wakati mwingine kujifungulia njiani kwasababu ya ubovu wa barabara.
“Kwakweli tunaishukuru sana Serikali yetu hii kwa kutupigania kwa kupata barabara zetu sasa hivi hadi kuna taa,kwakweli zamani tulikuwa tunapata shida sana kulikua na madimbwi sana na usafiri haukuwepo”.
Bw. Ramadhani Simba mkazi wa Kibaha-Zogoare ameishukuru Serikali kwani barabara hiyo ya lami imewarahisishia usafiri na sasa inapitika wakati wote.