Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke Mhandisi Ezekiel Mashola (kushoto) akipata futari iliyoandaliwa na TANESCO katika Ukumbi wa Maonesho Sabasaba leo Aprili 09, 2024 jijini Dar es Salaam.
Watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke wakiwa katika hafla ya Iftari aliyoandaliwa na TANESCO katika Ukumbi wa Maonesho Sabasaba leo Aprili 09, 2024 jijini Dar es Salaam.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imefuturisha watumishi wake wa Mkoa wa Temeke, huku wakiaidi kuendelea kudumisha umoja na mshikamano katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi kwa kutoa huduma bora kwa jamii.
Akizungumza leo April 9, 2024 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Gisima Nyamuhanga, katika hafla fupi ya Iftari iliyofanyika katika Ukumbi wa Maonesho Sabasaba, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke Mhandisi Ezekiel Mashola, amesema kuwa wafanyakazi wa TANESCO wamejipanga kuendelea kutoa huduma bora kwa kuhakikisha umeme unapatikana muda wote.
Mhandisi Mashola amesema kuwa ushirikiano katika kazi ni jambo la muhimu hivyo kupitia futari ya pamoja inakwenda kudumisha umoja kwa wafanyakazi kutoka Wilaya zote katika Mkoa wa Temeke.
“Tukio hili ni sehemu ya kutimiza lengo la Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO la kufuturisha wafanyakazi, tutaendelea kufanya kazi kwa ufasini ili huduma ya umeme ipatikane muda wote na kuchochea shughuli za maendeleo” amesema Mhandisi Mashola.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujenga tabia na mazoea ya kutunza miundombinu ya umeme, kwani kufanya hivyo itasaidia kupiga hatua katika maendelea kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Nao baadhi ya watumishi wa TANESCO Mkoa wa Temeke walioshiriki katika futari hiyo ikiwemo Luncy Mwaisemba pamoja na Nurdin Mali wamesema kuwa wamefarajika na kufurahishwa kutokana kuwa hafla hii imewaongezea hamasa ya kufanya kazi kwa ushirikiano.
“Tunamshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kwa kutufuturisha wafanyakazi wa Mkoa wa Temeke, tumeshiriki wafanyakazi wote wa Wilaya nne, tumefurai sana kwani ni tukio la kihistoria kwetu” amesema Mwaisemba.