Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Joseph Kailaga akitoa elimu Aprili 8, 2024 kwa watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani hapa iliyohusu madhara ya rushwa mahala pa kazi na athari zake.
Na Mwandishi Wetu, Singida
WATUMISHI wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
Mkoa wa Singida wametakiwa kuteleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya sheria,
kanuni, taratibu na miongozo iliyopo ili kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Joseph Kailaga aliyasema hayo Aprili 8, 2024 wakati
akitoa elimu kwa watumishi hao iliyohusu madhara ya rushwa mahala pa kazi na
athari za kuomba na kupokea rushwa.
Kailaga alisema pia TAKUKURU wameweza
kuwakumbusha wafanyakazi hao wanapotekeleza majukumu yao wafuate miongozo na
sheria ili kujiepusha na vitendo vyovyote vya rushwa na kuwa athari ya vitendo
hivyo ni kubwa sana katika jamii.
“Tumewataka watumishi hao wanapokuwa
wakiwaungania wananchi umeme wafuate taratibu na miongozo waliojiwekea katika
kutekeleza majukumu yao bila ya kujihusisha na vitendo vya rushwa, ”
alisema Kailaga.
Kailaga alisema TAKUKURU inawashukuru Tanesco kwa
kufanya maboresho ya wateja wao kutumia
mfumo wa kuomba maombi yao ya kuingiziwa umeme
kwa njia ya kielekritoniki ambayo imepunguza urasimu na vitendo vya
rushwa kwa kuonana na mtu mmoja mmoja ofisini na baada ya kujaza fomu ya maombi
ataenda kufanyiwa taratibu za kupimiwa na kuandikiwa michoro katika nyumba yake
na kuwekewa umeme.
Aidha, Kailaga alisema Serikali imeweka utaratibu
huo ambao umepunguza vitendo vya rushwa kwa watumishi wa Tanesco kwa kutumia
mfumo huo na wao kama TAKUKURU wamepongeza utaratibu huo.
Alisema watumishi hao wa Tanesco baada ya kupata
elimu hiyo wameahidi kuwa mabalozi wazuri kwa kutoshiriki vitendo vya rushwa na
kuwa watatekeleza majukumu yao kwa weledi na kufuata maadili ili kutokomeza
vitendo vya rushwa.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida Mhandisi
Mwamvita Ally akitoa mresho kwa watumishi hao kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Doto Biteko baada ya kufanyika kikao hivi karibuni jijini Mwanza aliwapongeza watumishi hao kwa uvumilivu wao katika kipindi kigumu
walichopitia cha mgao wa umeme ambapo waliweza kuwahudumia wateja wao vizuri
licha ya kuwepo kwa malalamiko mengi lakini walipambana hadi hali ya
upatikanaji wa umeme ilipokuwa nzuri.
Mhandisi huyo alisema mambo mengine aliyoyagiza kwa
watumishi hao ni jinsi shirika hilo lilivyokuwa limechafuka kwa vitendo
vya rushwa ambapo aliwata kutoka kwenye uchafu huo na kulisafisha ili jamii
iwe na imani nalo kwa kufanya kazi kwa kufuata maadili na kufuata sheria za
utumishi wa umma na kutoa lugha nzuri wanapowahudumia wateja wao.
Asiatu Mnanura akizungumza kwa niaba ya watumishi
wa shirika hilo aliwashukuru TAKUKURU na TANESCO kwa kuwapa elimu hiyo ambayo
imewaongezea uwezo mbalimbali wa kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuwa
wataendelea kukumbusha kuhusu jambo hilo na kuwa mabalozi wazuri wa kupinga
rushwa.