Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua Nembo ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, hafla iliyofanyika leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, amezindua nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Muungano huku akiwataka Watanzania wote,kuendelea kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Majaliwa, ameyabainisha leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa nembo na kaulimbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Mhe.Majaliwa amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia muungano wao kutimiza miaka 60.
“Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla ,Kama ulivyo msemo wa Kiswahili Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, muungano wetu umefanya Tanzania liwe Taifa lenye utulivu, mshikamano, nguvu na mfano kwa mataifa mengi Barani Afrika na duniani kwa ujumla.“amesema Mhe.Majaliwa
Pia amezitaka taasisi zinazotoa elimu, ziendelee kufundisha mada kuhusu muungano wetu kuanzia elimu ya awali ili watoto na vijana waufahamu na wawe walinzi na hatimaye wawe vinara katika kuundeleza.
Hata hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wote wa pande mbili za muungano wajitokeze kwa wingi ili kushuhudia kilele cha sherehe za Muungano katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam
“Wananchi wote tumieni maadhimisho haya kutafakari tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi tangu muungano uliopoasisiwa mwaka 1964. Kaulimbiu ya maadhimisho haya ituongoze katika tafakuri hiyo ili kwa pamoja tuendelee kuulinda na kuutetea muungano wetu.“amesema
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Watanzania wana kila sababu ya kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Amewataka Watanzania kutembea kifua mbele kujivunia Muungano huo adhimu ambao umeleta faida lukuki zikiwemo uhusiano mzuri baina ya wananchi wa pande zote mbili katika Nyanja mbalimbali.
Waziri Dkt. Jafo amewashukuru na kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa usimamizi wao na kuwezesha utatuzi wa changamoto 15 kati ya 18 ndani ya miaka mitatu ya uongozi wao.
“Leo hii tunaanza mbio za miaka 60 ya Muungano na hili ni jambo la kipekee tangu Muungano ulipoundwa, mwaka huu nchi yetu inatengeneza historia yake ya kipekee na sisi Ofisi ya Makamu wa Rais yale yote ambayo Watanzania walipaswa kujivunia tumejitahidi kufanya kila linalowezekana,” amesema Dkt. Jafo.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma amesema kuwa muungano huu ni tunu kubwa, hivyo kila Mtanzania anawajibu wa kuulinda, kuutunza na kuutetea kwa hali zote.
Amesema Tukio hili la uzinduzi wa nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linaenzi mawazo ya viongozi waasisi wa muungano wetu.
“Amewataka Watanzania kuwaenzi Waasisi wa Muungano Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ambaye Aprili 07, 2024 ilikuwa kumbukizi ya miaka 52 ya kifo chake.”amesema Mhe.Juma
Awali,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amesema Muungano huo ni sawa na Jubelei ya Almasi, hivyo, haina budi kukaa pamoja kama Taifa moja kumshukuru Mungu na kuiadhimisha kwa furaha miaka hiyo 60.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kabla ya kuzindua Nembo na Kaulimbiu ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hafla iliyofanyika leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,akisisitiza jambo kwa washiriki (hawapo pichani) kabla ya kuzindua Nembo na Kaulimbiu ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hafla iliyofanyika leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama,akielezea shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wakati wa uzinduzi wa Nembo na Kaulimbiu ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Nembo na Kaulimbiu ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Mhe. Hamza Hassan Juma ,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Nembo na Kaulimbiu ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.
Baadhi ya Mawaziri na Viongozi mbalimbali wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (hayupo pichani) akizungumza kabla ya kuzindua Nembo na Kaulimbiu ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hafla iliyofanyika leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua Nembo ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, hafla iliyofanyika leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.
Baadhi ya Mawaziri wakifatilia uzinduzi wa Nembo ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano,uliofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Aprili 8,2024 jijini Dodoma.