Na Mwandishi Wetu, Moshi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo Aprili 8, 2024, amefungua Semina Elekezi kwa watumishi wa ajira mpya 96 waliohitimu mafunzo ya awali ya Uhifadhi na kuwa tayari kuanza majukumu yao kama watumishi wa umma.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kufanyika katika Chuo cha Viwanda na Misitu (FITI) mjini Moshi yanalenga kuwaandaa vijana hao kuanza majukumu yao ya Utumishi wa Umma wakiwa na maadili na kuijua misingi ya utumishi wao.
Akizungumza katika ufunguzi huo Dkt. Abbasi amewaasa kuzingatia maadili watakapokuwa kazini, kufanya kazi kwa bidii na kujiwekea malengo makubwa.
“Pamoja na mambo mengine niliyowaeleza yatakayowasaidia kufika mbali suala la maadili ndio msingi mkuu. Mnakwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo mbalimbali ya misitu nchini ni matarajio yetu mtawahudumia wananchi na pale wanapokosea kuwaelimisha badala ya kutumia nguvu au kupokea rushwa kuacha raslimali zikiharibiwa. Binafsi nikisikia hayo kwenu nitasikitika sana na tutachukua hatua kali”, alisema Dkt. Abbasi.
Akiwa Chuoni hapo pia ametembelea Chuo cha Viwanda na Misitu (FITI) na kuzungumza na wafanyakazi ambapo amewaeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inakijali mno Chuo hicho na mipango ya kukiboresha imeanza ikiwemo kuongezewa bajeti kwa zaidi ya asilimia 100 katika mwaka wa fedha utakaoanza Julai, 2024.