Viongozi wa dini ya kiislam wilayani Ilemela mkoa wa Mwanza wamekemea utaratibu wa kualika iftar zisizofuata sheria na taratibu za dini walizoziita Iftar za fashion
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ilemela wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania BAKWATA Shekh Mohamed Idd Uledi ambapo ameitaka jamii kuacha kualikana iftar katika maeneo yasiyofaa kama bar na kumbi nyenginezo za starehe pamoja na kufuturisha vitu vilivyoharamishwa na dini hiyo ikiwemo vileo
‘.. Wapo baadhi ya watu siku hizi wanaalika watu kwenye futari fashion, Wanakuitia bar na wanaweka na bia katika futari zao, Hakuna iftar ya bia katika uislam na hapo hapo anataka na fataha isomwe ..’ Alisema
Aidha Shekh Uledi amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuzingatia sheria na taratibu za kiislam Kila mwaka anapoandaa iftar kwa makundi ya watu wasiojiweza yakiwemo makundi ya mayatima, wajane, wagane, wazee, masikini, mashekh, maimam, pamoja na kushirikisha viongozi wa dini hiyo katika maeneo yao
Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Hasan Milanga amempongeza na kumshukuru Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusaidia makundi hayo yaliyosahaulika katika jamii licha ya yeye binafsi kuwa mkristo amekuwa akiheshimu dini nyengine na kushirikiana nazo katika kutekeleza matendo ya imani zao
Nae Mbunge wa Jimbo hilo Dkt Angeline Mabula mbali na kumshukuru Mungu kwa mwezi mtukufu wa Ramadan kufuatana na mfungo wa Kwaresma, amefafanua kuwa anatambua uhitaji wa makundi yaliyo katika jamii na kwamba ameweka nadhiri ya kuhakikisha Kila mwaka kufuturisha makundi maalum ya wazee, mayatima, wajane, wagane na watu wengine wasiojiweza hata kwa kugawa mahitaji ya chakula vikiwemo mchele, sukari, ngano na tambi huku akiwashukuru wadau wa maendeleo waliomuunga mkono katika kufanikisha zoezi hilo la kugawa iftar wakiwemo taasisi ya The Angeline Foundation, GBP, AFROIL, Nyanza Road Works Co Ltd na Superdoll
Zaidi ya waumini 520 na misikiti 39 inayopatikana ndani ya Jimbo hilo wameshiriki zoezi la kupokea sadaka ya iftar kutoka Kwa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula lililofanyika katika ukumbi wa chuo cha maliasili na wanyamapori Pasiansi ambapo wamepokea mchele, sukari, ngano na tende kila mmoja