Timu ya madaktari bingwa wabobezi wa upasuaji kutoka nchini Marekani imewasili mkoani Katavi kwa lengo la kutoa huduma za upasuaji bure kwa wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji wa magonjwa mbalimbali.
Timu hiyo ya wataalamu 18 wakiwemo madaktari bingwa wanne, watoa dawa za usingizi wawili na wasaidizi wao watatoa huduma hizo katika hospitali ya wilaya ya Tanganyika iliyopo Majalila.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya madaktari hao kutua katika uwanja wa ndege wa Mpanda, Mganga Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Dk. Alex Mrema alisema mdaktari hao watatoa huduma hadi tarehe 13 mwezi huu.
Dk. Mrema aliongeza kuwa wameshaanza kupokea wagonjwa na kuwafanyia uchunguzi na kutoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Katavi kuitumia fursa hii vizuri.
Profesa Eddie Chan ni Kiongozi wa timu hiyo ya madaktari, alisema wamefurahi kufika Tanzania na kuahidi kutoa huduma bora kwa wagonjwa watakaowahudumia.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Juma Shabani alisema hii ni awamu ya kwanza ya ujio wa madaktari hao bingwa na wanategemea kupokea madaktari wengine mapema mwezi Mei.
Awali Mkuu wa wilaya hiyo Onesmo Buswelu aliwataka wakazi wa Tanganyika na Katavi kwa ujumla kujitokeza kupata matibabu.