Na MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, ametaka imani za dini ziendelee kutumika kuwunganisha Watanzania, kuhamasisha, amani, umoja na mshikamano.
Aidha, amewasisitiza Watanzania kuutumia mwezi mtukufu wa Ramadhan kuwa jukwaa la kuwaelimisha na kuwaunganisha kushikamana na kuleta maelewano.
Shaka ameyasema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kigoma Malima alipomwakilisha katika mashindano ya kuhifadhi Qur’an yalioshirikisha washiriki kutoka mikoa ya Morogoro, Pwani na Iringa yaliofanyika katika viwanja vya Msikiti wa Bomani mjini Morogoro.
Alisema kuwa kila Mtanzania aelewe kuwa taifa halina dini bali wananchi wake ndiyo wenye kufuata imani mbalimbali, hivyo kila mmoja ana fursa ya kuabudu kulingana na Imani yake.
“Kila mtanzania nchi yetu inamtambua ni binadamu anayestahili heshima na haki kwa mujibu wa katiba yetu. Taifa letu katiba yake imempa Uhuru wa kuabudu bila kuvunja mpaka, Kikitokea chama au kundi lenye lengo la kuvuruga amani na kupandikiza chuki lilaaniwe na jamii ya watanzania “Alisema Shaka.
“Tunahitaji kumshuhudia kila mwananchi akipanda mbegu za amani, umoja na upendo, tunamshukuru Mungu tune Rais Samia mwenye hofu ya Mungu kazi kubwa anaiyoifanya kutunganisha kama Taifa inahitaji kuungwa mkono na kila mmoja wetu ili kuchochea maendeleo endelevu ndani ya nchi,” alisema Shaka.
Aidha aliwataka viongozi wa dini waendelee na kazi ya kuipika mioyo ya waumini wao huku wakiwahimiza na kuwaeleimisha fadhila na neema za kumuamini Munngu, kuendeleza upendo na kuwajali wenye dini na hata wasio na dini.
“Nawahusia muufanye mwezi huu mtukufu wa Ramadhan uwe jukwaa la uadilifu linalotoa elimu itakayowajengea maarifa waumini na wasio na dini .Viongozo wa dini zote waendelee kuhubiri upendo ndani na nje ya nyumba za ibada . Misikiti na Makanisa yaendelee na kazi ya kuelimisha imani na umoja ” Alisema katibu huyo.
Alisema kila muumini wa dini anahitaji kupata nafasi ya kumuabudu mola wake akiwa katika mazingira ya amani kwani utulivu , amani na umoja ukitoweka huwa mwanzo mitafaruku na vurugu zitakazowanyima waumini wakose muda wa kufanya ibada zao kwa utuamo.
Akizungumza kadhi wa mkoa wa Morogoro Mohamed Masenga amesifu jitihada za viongozi wa serikali katika kuwaunganisha watanzania jambo ambalo nchi imeendelea kuwa na amani upendo na umoja huku wakishuhudi mipango mbali mbali ya kuletea maendeleo ikifanikiwa.
Mashindano hayo ya Qur’an ni mwendelezo wa shughuli inayofanyika kila mwaka ambapo imeshirikisha washiriki kutoka mikoa ya Iringa, Morogoro na Pwani na kwa mwaka huu Shaka Hamdu Shaka amekubali kuwa mlezi wa mashindano ambapo washindi walikabidhiwa zawadi mbali mbali.