Na Ashrack Miraji
Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amesema jumla ya miradi nane (08) ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 3.6 inatarajiwa kupitiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 ikiwemo ya barabara, vijana, elimu, maji, afya pamoja na mazingira.
Akizungumza na mwaandishi wetu ofisin kwake Leo Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha hayo wakati akitoa taarifa ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 ambao utapokelewa kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Njoro asubuhi ya April nane (08) ukiwa unatokea na Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.
Aidha DC Kasilda Mgeni amesema baada ya kuupokea Mwenge utakimbizwa Wilayani humo Kilometa 138.4 katika mbio hizo miradi minne (04) itafunguliwa, mitatu (03) itatembelewa na mmoja (01) utawekewa jiwe la msingi ambao ni mradi wa kwanza wa barabara uliopo same mjini.
“Niwaombe wananchi wote ambao wapo Wilayani Same wahakikishe wanajitokeza kwa wingi Shule ya Msingi Njoro kuupokea Mwenge wa Uhuru kwa shamla shamla, nderemo na vifijo lakini pia kujitokeza kwa wingi kwenye mkesha wake pale uwanja wa Shule ya Msingi Hedaru.”
Pia amesema kuwa maandalizi muhimu ya kuupokea Mwenge huo tayari yamekamilika ikiwemo miradi ya maendeleo itakayopitiwa lakini pia jukwaa la viongozi pamoja na la wasanii kwenye eneo la mkesha wa Mwenge ambapo imepangwa kufanyika viwanja vya Shule ya Msingi Hedaru.
Nao baadhi ya viongozi wa madhehebu dini Wilayani humo wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti wamesema kuwa wananchi wanapaswa kutambua kufika kwa mwenge Wilayani humo ni moja ya sehemu ya maendeleo kwao kwani miradi mbali mbali ya maendeleo itafunguliwa hivyo hawanabudi kujitokeza kwa wingi kusikiliza maelekezo muhimu kutoka kwa viongozi wa mbio za Mwenge kitaifa.
Kwa mwaka 2024 mbio za Mwenge wa Uhuru zimebeba kaulimbiu isemayo “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.