Tanzania Msumbiji zakubaliana kuanzisha mchakato wa kusainiwa Hati ya Mkubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya TIC na APIEX.
Makubaliano hayo yalifikiwa tarehe 03 Aprili, 2024 wakati Mhe. Phaustine Kasike, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji alipokutana na Bw. Gil Bires, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kukuza Uwekezaji na Usafirishaji wa Bidhaa za Msumbiji Nje ya Nchi (Investment and Export Promotion Agency – APIEX) kwenye Ofisi za Wakala huyo Jijini Maputo.
Katika Mkutano huo, Bw Bires alikubaliana na pendekezo lililotolewa na Mhe. Balozi Kasike la kuanzishwa ushirikiano huo mapema hasa kwa kuzingatia uhusiano wa kihistoria na ukaribu wa kijiografia baina ya nchi hizi mbili.
Awali, Mhe. Balozi Kasike alieleza kwamba kwa muda mrefu Tanzania na Msumbiji zimekuwa na uhusiano mzuri katika nyanja za kisiasa na kijamii, hivyo ni vyema uhusiano huo ukaelekezwa pia kwenye nyanja ya Kiuchumi ili kusaidia kuleta maendeleo endelevu kwenye nchi hizo mbili.
Katika kutekeleza suala hilo, alisisitiza umuhimu kwa TIC na APIEX kuanza mchakato wa kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) itakayowezesha Taasisi hizo pamoja na masuala mengine; kurasimisha ushirikiano huo, kubadilishana utaalamu na uzoefu, kushirikiana katika kuandaa Matamasha na Matukio mengine yanayohusu Sekta ya Uwekezaji pia kubainisha maeneo mahususi ya ushirikiano.