“Asema DC Rufiji Mej. Edward Gowelle*
*Asema utolewaji taarifa mapema umesaidia kuokoa maisha ya wananchi kwani hakuna kifo kilichoripotiwa kutokea
*Awasihi watu kuacha kupotosha ukweli kuwa ujenzi wa Bwawa la JNHPP ndio sababu pekee ya mafuriko
*Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ukanda wa nyanda za juu kusini zatajwa sababu kubwa ya kuongezeka wingi wa maji JNHPP
*TANESCO yapiga kambi wilaya ya Rufiji kuelimisha wananchi
Na Charles Kombe, Rufiji
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowelle amesema kuwa mradi wa kufua umeme wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) umepunguza kwa kiasi kikubwa mafuriko na athari zake yaliyokuwa yakitokea katika wilaya hiyo.
Meja Gowelle ameyasema hayo 05.04.2024 katika mazungumzo yake na wawakilishi kutoka Shirika la Umeme, TANESCO, walipotembelea wilayani kwake baada ya kukagua, kujionea na kufanya tathmini ya athari mbalimbali zilizojitokeza kutokana na mafuriko yaliyotokea.
Amesema kuwa kujengwa kwa JNHPP lilikuwa wazo zuri na kumerahishisha kitaalamu kujua kiwango cha maji kinachotolewa kwenda kwa wananchi na hivyo kufanya athari kuwa ndogo ikilinganishwa na namna ilivyokua wakati bwawa halijajengwa ambapo mafuriko yalikua yanatokea bila kujua kiwango cha mtiririko wa maji.
“Miaka hiyo ya nyuma kulikuwa hakuna tahadhari. Wananchi walikuwa wakijishtukia tu maji yamejaa katika nyumba zao na mashamba yao. Kipindi hiki sisi kama serikali tuliweza kupata tahadhari ya mapema kutoka TANESCO hivyo tuliweza kufikisha taarifa kwa wananchi na kuwezesha kujinusuru. Na ndio maana mpaka sasa hakuna kifo hata kimoja kilichoripotiwa kutokea kutokana na maji” alisema Meja Gowelle.
Ameeleza kwa kiasi kikubwa tahadhari na taarifa zilitolewa mapema kwa wananchi na hvyo kusaidia kupunguza athari kwenye maisha ya watu ukilinganisha na mashamba ya mazao mbalimbali kama mahindi,mpunga nk kuharibika.
Nae mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji Bwn Abdul Bakari Chobo amesema mafuriko Rufiji ni suala la miaka mingi tangu yeye anazaliwa anakua akiyaona lakini ni ukweli dhahiri kwamba Bwawa la Julius Nyerere limepunguza makali ya mafuriko kwani hawakuwahi kupata mafuriko kabisa miaka ya hivi karibuni.
”kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha kwenye ukanda wa nyanda za juu kusini maji yamekua mengi na hivyo iwapo Bwawa lisingekuwepo huenda madhara yangekua makubwa zaidi nawasihi watu kuacha upotoshaji wa taarifa kuwa sababu kubwa ya mafuriko ni ujenzi wa bwawa tunatumaini litakapokamilika litapunguza zaidi athari hizi na kwa sisi kama Rufiji mradi umetusaidia mambo mengi sana sana tunapata service levy tumejenga mashule nk’.
Kwa upande wake Mtendaji kata ya Muhoro ,Helda Kuboja ameipongeza TANESCO kwa ushirikiano mkubwa inaoendelea kuutoa katika eneo hilo.
“TANESCO wameendelea kuangalia na kuchukua tahadhari pale ambapo kunatokea shida yoyote. Mfano tulikua na changamoto ya nguzo kuanguka kipindi hiki cha mafuriko ambapo walifika kwa haraka na kuhakikisha nguzo zile zinaondolewa wananchi wanapata umeme na haijaleta madhara yoyote kwa wananchi.
Aidha Kuboja amesema kuwa TANESCO imeendelea kuwepo katika eneo hilo kila siku na kufuatilia pamoja na kujua na kuchukua tahadhari zozote ambazo zinaweza kujitokeza.
Yusuph Mbawala ni mwalimu wa Shule ya Msingi Mohoro wilayani Rufiji aliyeishi katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 10 amesema kuwa marufiko yamekuwa yakishuhudiwa maeneo hayo hata kabla ya ujenzi wa JNHPP.
“Kutokea mara kwa mara kwa mafuriko haya sio tu kwasababu ya uwepo wa lile bwawa kwakua hata kabla ya uwepo wa bwawa mafuriko haya yalikuwa yanatokea. Yalitokea 2016 yakatokea 2020, kwahiyo ni kama mwendelezo wa mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara lakini uwepo wa JNHPP ni afueni kubwa kwa sisi wakazi wa Rufiji” anasema Mbalawa
Kwa upande wake mkurugenzi wa kanda ya mashariki na msemaji wa TANESCO, Mhandisi Kenneth Boymanda amesema ujenzi wa Bwawa umesaidia sana kupunguza athari za mafuriko ambapo katika maeneo hayo mara ya mwisho kuonekana mafuriko ilikuwa mwaka 2021 kutokana na uwezo wa Bwawa kuhifadhi maji yaliyosaidia wananchi kutopata mafuriko miaka ya nyuma na amewaasa wananchi kuendelea kuchukua kila aina ya tahadhari ili kuepuka madhara yanayoweza kuzuilika.
”Shirika linaendelea kutoa tahadhari kwa wakazi wote wanaoishi kwenye ukanda wa chini wa wilaya za Rufiji na Kibiti juu ya ongezeko la maji. Ni vyema wananchi wengi hasa wale wanaoishi kwenye yale maeneo ambayo mara zote yamekuwa yakikumbwa na mafuriko kuchukua tahadhari ili kuokoa mali zao na uhai wao na pasitokee majanga makubwa ambayo yangeweza kuzuilika” amesema Boymanda.
Nae mhandisi wa maji kutoka mradi wa Julius Nyerere Dismas Mbote amesema licha ya kuanza kutoa elimu ya kutosha kabla ya ufunguliaji wa maji bado timu ya wafanyakazi wa mradi wa JNHPP inaendelea kupiga kambi maeneo hayo kuhakikisha wananchi wanaondoka salama .
“Tuko huku kujibu maswali ya wananchi, kutoa ufafanuzi na kurekebisha maneno ambayo kuna watu wasio na nia njema wanapotosha ukweli na kutaka kuigombanisha Serikali na wananchi. Na sisi tunawaelimisha na kuwapa ukweli na Wananchi wengi wanatuelewa na wao wanakiri kwamba mafuriko haya yamekuwepo kwa miaka mingi na yamekuwa yakija na kupita” amesema Mha. Mbote.
Zoezi la kupunguza maji katika bwawa la Nyerere lilianza rasmi Machi 8, 2024 na bado linaendelea kadri kina cha maji kinavyoonekana kuzidi huku likiendelea kupunguza kiasi cha maji yaliyopaswa kwenda kwa wananchi katika wilaya ya Rufiji.