Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata akizungumza na wadau mbalimbali katika hafla ya kufuturisha iliyofanyika leo April 5, 2024 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na wadau mbalimbali wakipata futari iliyoandaliwa na TRA
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewafuturisha wadau mbalimbali, huku wakiaidi kuendelea kufanya kazi kwa uweledi, uwazi, uaminifu mkubwa jambo ambalo litasaidia kukusanya mapato ya Serikali kwa ufanisi na kulijenga Taifa bila kuvunja kanuni na taratibu zilizowekwa kwa kuzingatia sheria.
Akizungumza leo Aprili 5, 2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kufuturisha wadau mbalimbali, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata, amesema kuwa watanzania wanapaswa kuwa wakweli na wadilifu katika ulipaji wa kodi ili kuleta tija kwa Taifa.
“Ukweli, uwajibikaji, uadilifu pamoja na ushirikiano na wadau mbalilmbali unatakiwa katika kazi ili kuleta matokeo chanya katika kukusanya mapato ya serikali” amesema Kamishna Kidata.
Amesema kuwa wanafuraha kubwa ya kukutana na familia ya TRA katika futari ya pamoja ambayo imewajumuisha watumishi wa TRA pamoja na wadau.
Kamishna Kidata amesisitiza umuhimu wa kuzidisha ibada, kuimarisha umoja na mshikamano, huruma na upendo pamoja na kuwasaidia wahitaji katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Sisi wote ni wamoja na tunatimiza maelekezo ya Mwenyezi Mungu ya kuishi kwa upendo, huku kila mmoja anapaswa kutambua umuhimu wa mwenzake” amesema Kamishna Kidata.
Amefafanua kuwa ni nzuri kwa TRA kufuturu pamoja na wadau kwani ni fursa ya kubadilishana mawazo, kuimarisha ushirikiano pamoja na kutatua changamoto zilizopo.