Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro, Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Denmark, Mhe. Dan Jørgesen, baada ya kukutana jijini Dodoma na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja za uwekezaji kwa kuishirikisha Sekta binafsi, Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na masuala ya kiuchumi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza wakati wa Mkutano na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Denmark, Mhe. Dan Jørgesen (hayupo pichani) aliyeambatana na ujumbe wake, ambapo wamefanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja za uwekezaji kwa kuishirikisha Sekta binafsi, Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na masuala ya kiuchumi, jijini Dodoma.
Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Denmark, Mhe. Dan Jørgesen, akizungumza wakati wa Mkutano wake na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), ambapo wamefanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja za uwekezaji kwa kuishirikisha Sekta binafsi, Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na masuala ya kiuchumi, jijini Dodoma.
Ujumbe wa Tanzania (kulia) ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Ujumbe wa Serikali ya Denmark (kushoto) ulioongozwa na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa nchi hiyo, Mhe. Dan Jørgesen, wakifanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja za uwekezaji kwa kuishirikisha Sekta binafsi, Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na masuala ya kiuchumi, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na Ujumbe wa Serikali ya Denmark ulioongozwa na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa nchi hiyo, Mhe. Dan Jørgesen (hayupo pichani), ambapo pande zote mbili zilijadiliana namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja za uwekezaji kwa kuishirikisha Sekta binafsi, Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na masuala ya kiuchumi, jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania katika nchi za Scandinavia, Dkt. Grace Olotu ( wa kwanza kushoto), Balozi wa Heshima nchini Denmark, Mhe. Simon Mears ( wa kwanza kushoto nyuma), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa tatu kushoto), Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Madeni – Wizara ya Fedha, Bi. Tiba Kisonga (wa pili kushoto), Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. Melckzedeck Mbise na Kamishna Msaidizi wa Sera Wizara ya Fedha, Dkt. Cyril Chimilila (wa pili kulia).
Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Denmark, Mhe. Dan Jørgesen, akisaini Kitabu cha wageni katika ofisi ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), jijini Dodoma, alipofika na ujumbe wake kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili ambapo mjadala ulijielekeza namna ya kutekeleza mkakati mpya unaoandaliwa na Denmark kwa ajili ya sera zake za uhusiano wa mambo ya nje ambapo mwelekeo mkubwa kwa Tanzania utakuwa kushirikiana katika nyanja za uwekezaji kwa kuishirikisha Sekta binafsi, Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na masuala ya kiuchumi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Denmark, Mhe. Dan Jørgesen (wa sita kushoto), Naibu Waziri wa Maendeleo wa Serikali ya Denmark, Mhe. Lotte Machon (wa nne kushoto), Balozi wa Tanzania katika nchi za Scandinavia, Dkt. Grace Olotu (wa nne kulia), Balozi wa Tanzania wa Heshima nchini Denmark, Mhe. Simon Mears ( wa pili kulia), Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Dissing-Spandet ( wa tano kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa sita kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wengine wa nchi hizo mbili baada ya kumaliza mkutano wao, ambapo wamejadiliana kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja za uwekezaji kwa kuishirikisha Sekta binafsi, Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na masuala ya kiuchumi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Kushoto), akiagana na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Denmark, Mhe. Dan Jørgesen, baada ya kumaliza mkutano wao jijini Dodoma, ambapo walijadiliana kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja za uwekezaji kwa kuishirikisha Sekta binafsi, Nishati, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na masuala ya kiuchumi. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maendeleo Serikali ya Denmark, Mhe. Lotte Machon, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Dissing-Spandet, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Balozi wa Tanzania katika nchi za Scandinavia, Dkt. Grace Olotu, na Balozi wa Tanzania wa Heshima nchini Denmark, Mhe. Simon Mears na Viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali ya Denmark (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
………
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameihakikishia Denmark kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi hiyo kupitia Mkakati wake mpya wa ushirikiano wa kimataifa kwa kuishirikisha sekta binafsi katika mipango yake ya maendeleo ili kukuza uchumi na ajira.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgesen, jijini Dodoma.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania ina fursa kubwa za uwekezaji katika sekta mbalimbali na kutoa wito kwa kampuni, mashirika na Taasisi mbalimbali kutoka Denmark kushirikiana na sekta binafsi ya Tanzania kuwekeza mitaji na teknolojia ili pande zote mbili ziwezeze kunufaika.
Alisema kuwa mkazo mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kuwa Sekta binafsi ndiyo inayotakiwa kuendesha uchumi wa nchi na kwamba ili kufanikisha mpango huo, Serikali imefanya mageuzi makubwa ya kisera na kisheria ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Dkt. Nchemba aliyataja baadhi ya maeneo yanayohitaji ushiriki wa sekta binafsi kuwa ni pamoja na uendeshaji wa reli ya kisasa ya SGR, masuala ya nishati, kilimo, na maeneo mengine kadha wa kadha.
Alisema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Denmark kupitia mpango wake mpya wa ushirikiano baada ya kusitisha uamuzi huo wa kufunga ubalozi wake nchini ambapo nchi hiyo imepanga kuongeza kiwango cha ufadhili na kuelekeza fedha hizo kwenye maeneo yatakayokuza uchumi, ikiwemo nishati, kuboresha mifumo ya kodi, kilimo, elimu, afya, pamoja na kusaidia sekta binafsi.
Dkt. Nchemba alirejea shukrani zake kwa Denmark kwa kuendeleza ushirikiano wake uliotimiza miaka 60, ambapo katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizo mbili zilikuwa zikitekeleza miradi ambayo Denmark iliipatia Tanzania msaada wa takriban Denish Krone bilioni 2, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 646.
Aidha, alisema kuwa Denmark kupitia Shirika lake la Maendeleo (DANIDA), imetoa zaidi ya shilingi bilioni 103 zinazotokana na mapato ya uwekezaji wake wa hisa katika Benki ya CRDB, ambazo zimetumika kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya kupitia Mfuko wa Afya.
Aliiomba pia Denmark kupitia Taasisi yake inayohusika na masuala ya Bima na Dhamana (Danish Export Credit Agency), kushiriki katika ujenzi wa mradi wa SGR kwa vipande vilivyobaki kutokana na umuhimu wa mradi huo katika kukuza biashara na ustawi wa maisha ya watu watakao tumia reli hiyo pamoja na kukuza pato la Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Denmark, Mhe. Dan Jørgesen, alimpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Sukuhu Hassan, kwa hatua kubwa ambayo nchi imepiga kiuchumi licha ya ulimwengu kukabiliwa na changamoto mbalimbali na kwamba anaiona Tanzania kuwa moja ya nchi kubwa kiuchumi kwa siku zijazo.
Aliishauri Tanzania, kuishauri Denmark namna ya kuboresha ushirikiano na maeneo ya kimkakati ambayo nchi inataka kuyapa kipaumbele hususan katika eneo la uwekezaji na biashara katika mpango wake mpya wa ushirikiano na nchi za Afrika ambao nchi yake inauandaa na wanatarajia utazinduliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amealikwa kuitembelea nchi hiyo.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Maendeleo wa Serikali ya Denmark, Mhe. Lotte Machon, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Dissing-Spandet, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Balozi wa Tanzania katika nchi za Scandinavia, Dkt. Grace Olotu, na Balozi wa Tanzania wa Heshima nchini Denmark, Mhe. Simon Mears na Viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali ya Denmark.