Kaimu Naibu Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba akifungua semina ya siku moja kuhusu Kupambana na Kuzia Rushwa mahali pa kazi kwa wafanyakazi wa Ndaki hiyo. semina hiyo iliyoandaliwa na Uongozi wa Ndaki ya Dar es Salaam na kuwasilishwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU-Ilala.
Mkuu wa Idara ya Huduma za Utawala Bi. Janeth Mumangi akielezea umuhimu wa mafunzo hayo Kwa watumishi.
Afisa Mawasiliano WA TAKUKURU Ilala Bi. Immaculate Ngoti akifafanua zaidi njia za kujiepusha na rushwa.
Mkuu wa Uelimishaji Umma kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ilala Bi. Nerry Mwakyusa akizungumza wakati WA Semina ya kupambana na rushwa mahali pa kazi kwa watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam
Watumishi wa Ndaki ya Dar es Salaam katika picha na Kaimu Naibu Rasi Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba (katikati) baada ya kufunga Semina ya kupambana na kuziia rushwa mahali pa kazi. Kushoto ni Mkuu wa Uelimishaji Umma TAKUKURU Ilala Bi. Nerry Mwakyusa na Kulia ni Mkuu wa Idara ya Huduma za Utawala Ndaki ya Dar es Salaam Bi. Janeth Mumangi
………
Kaimu Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba amewakumbusha watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es salaam kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao kama watumishi wa umma ili kuepuka kuingia katika vitendo vya rushwa.
Dkt. Komba ameyasema wakati akifungua semina ya siku moja ya elimu ya mapambano dhidi ya rushwa mahala pa kazi iliyoandaliwa na uongozi wa Ndaki na kuendeshwa na Maafisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ilala Dar es salaam.
“Ni muhimu kukumbushana hata kama bado hatujabaini uwepo wa rushwa miongoni mwetu. Ninawaomba wafanyakazi wenzangu tuzingatie yale tukakayofundishwa ili tuweze kuepuka kuingia katika vitendo vya rushwa katika utendaji kazi wetu huu wa utumishi wa umma” Alisisitiza Dkt. Komba”
Mkuu wa Uelimishaji Umma TAKUKURU Ilala Bi. Nerry Mwakyusa amesema miongoni mwa sababu zinazofanya watumishi wa umma kujiinginza kwenye vitendo vya rushwa ni pamoja na mmomonyoko wa maadili, ubinafsi na tamaa ya kupenda kujilimbikizia mali pamoja na tamaa ya mwili ambayo hupelekea rushwa ya ngono.
Bi. Mwakyusa amesema taarifa za tafiti mbalimbali zinaoonesha kuwa rushwa vyuoni inaweza ikatokea wakati wa udahili ambapo kutokana na ufinyu wa nafasi katika vyuo bora wanafunzi hutoa rushwa ili waweze kupata upendeleo wa kudahiliwa.
Aidha, Bi. Mwakyusa ametaja maeneo mengine ni wakati wa mitihani ambapo wanachuo wasio waadilifu hutoa hongo kwa wahadhiri ili wapewe alama za juu kwenye mitihani kinyume na uwezo wao. Pia, ameyataja maeneo mengine kuwa ni wakati wa kuajili na wakati wa kupanda vyeo.
Naye Afisa Mawasiliano TAKUKURU Ilala, Bi Immaculete Ngoti amefafanua kuwa njia pekee ya kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa watumishi wa umma ni kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kanuni zake ambazo ni kutoa huduma bora, kutii Serikali iliyoko madarakani, kufanya kazi kwa bidii na uadilifu bila upendeleo na kutii sheria za nchi ikiwemo sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.
“Kupambana na rushwa si jukumu la serikali au TAKUKURU peke yake bali kila Mtanzania anao wajibu wa kushiriki ipasavyo katika kupambana na rushwa ikiwamo kutoa taarifa za vitendo vya rushwa TAKUKURU na kuwa tayari kutoa ushahidi mahakamani pale inapotakiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma za Utawala Ndaki ya Dar es Salam Bi. Janeth Mumangi amesema semina kama hizo ni vema zitolewe kila mara kwa lengo la kuwakumbusha na kuwapa uelewa watumishi katika kupambana na masuala ya rushwa sehemu za kazi ili kuboresha utendaji wa watumishi; hasa ukizingatia kwamba Chuo karibia kila mwaka kinaajiri watumishi wapya ambao huhitaji mafunzo hayo