Na Takdir Ali. Maelezo. 29/03/2024.
Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Magharibi Mhe. Tauhida Galos Nyimbo amesema Wazee wanakabiliwa na Changamoto mbalimbali ikiwemo maradhi na ugumu wa maisha hivyo wanahitaji kusaidiwa ili wasijihisi kuwa wametengwa na jamii.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea Wazee na Wagonjwa kwa Majimbo ya Wilaya ya Mfenesini kichama amesema Wazee hao wametoa mchango mkubwa katika mustakbali mwema wa Chama na Serikali na kueleza kuwa wanahitaji kuungwa mkono kwa hali na mali.
Amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kuwapa moyo, kuwafariji na kuwaunga mkono Wagonjwa na Wazee katika maeneo mbalimbali ili wajihisi kuwa sawa kama Watu wengine.
Hata hivyo ameahidi kuzidi kushiriana na kuwa kitu kimoja na Wazee hao ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuhakikisha Wazee wanaishi katika maisha bora katika maeneo yao na kuwaomba Wafadhili na Watu wenye uwezo kujitokeza kuwasaidia Wazee hao kwa faida yao na Taifa kwa Ujumla.
Mapema Katibu wa UWT Mkoa wa Magharibi kichama Fatma Ali Ameir amesema wameamua kuwa karibu na Wazee hao ili kuwafariji na kuwaombea dua jambo ambalo limewapa moyo Wazee hao kwani wamejihisi kuwa wapo pamoja na Viongozi wao.
Aidha amesema kutokana na Chama Cha Mapinduzi kuwajali na kuwaenzi Waasisi wa Chama hicho, Viongozi mbalimbali wameweka utaratibu wa kufanya ziara ya kuangalia Wazee na Wagonjwa katika maeneo yao kwa mustakbali wa Wazee hao na Chama kwa Ujumla.
Nao Wagonjwa na Waasisi wa Chama Cha Mapinduzi katika Wilaya hiyo wameomba Viongozi kufanya ziara za mara kwa mara kuwaangalia hasa Wanachama wa ngazi za Chini kwani wanakabiliwa na matatizo mbalimbali yanayohitaji kutatuliwa.