Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein M. Bashe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano Mkuu wa Jukwaa la wadau wa Chai unatarajiwa kufanyika Jijini Dodoma siku ya Jumanne Machi 26, 2024 ambapo mkutano huo utahudhuriwa na wadau mbalimbali wa zao la Chai.
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Chai Tanzania imesema Wadau wakuu wa zao la Chai watakaoshiriki katika mkutano huo ni wazalishaji (Wakulima wadogo, wa kati na wakubwa), wachakataji, wachanganyaji, wafungashaji, wafanyabiashara wa ndani, wauzaji nje, waingizaji nchini, watunga sera (Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais – TAMISEMI), wasimamizi wa utekelezaji wa Sera (Taasisi mbalimbali za Serikali, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji/Wilaya).
Taarifa hiyo imetaja wadau wengine kuwa ni Vyama vya ushirika na asasi za kiraia zilizoko katika mnyororo wa thamani wa zao la Chai na wabia wa maendeleo.
Aidha Taasisi za Serikali zinazojishughulisha na zao la Chai ambazo pia zinashiriki katika mkutano huu ni pamoja na Bodi ya Chai Tanzania (TBT), Wakala wa maendeleo ya Wakulima wadogo Tanzania (TSHTDA), Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT), Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Mamlaka ya udhibiti wa afya ya mimea na viuatilifu (TPHPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Taasisi rasmi ya ithibati ya Mbegu Tanzania (TOSCI) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA).
Washiriki wengine ni Wakuu wa Wilaya na Halmashauri zenye wakulima wa Chai nchini (Rungwe, Busokelo, Njombe, Ludewa, Mufindi, Kilolo, Muheza, Korogwe, Lushoto, Muleba, Bukoba na Tarime).
Pia Chama Kikuu cha ushirika cha wazalishaji wa Chai Tanzania (TASTGCU) na vyama vya ushirika vilivyoalikwa vinatoka mikoa yenye wakulima wa Chai ikiwemo Mbeya (RUBUTCOJE na ROTCO), Njombe (NJOTCOJE, MUVYULU na LUWIKA), Iringa (MUTCOJE na Kilolo AMCOS), Tanga (UWACHA, ZEMA, Sakare AMCOS, TAFU, Mponde, Kwemihafa na Kweminyasa), Tarime (WAMACU) na Kagera.
Mkutano huo hufanyika mara moja kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha wadau wote wa ndani na nje ya Tanzania kwa ajili ya kujadiliana kuhusu mafanikio, changamoto na fursa ili kubuni, kujadili na kuweka mikakati ya kuendeleza tasnia ya chai.
Katika mkutano wa jukwaa la wadau wa mwaka 2024, mada Kuu zitakazojadiliwa ni pamoja na:-
Kupitia muhtasari na taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano mkuu wa wadau wa zao la Chai uliofanyika Januari 18, 2023 Mkoani Iringa, Mkutano ambao ulijadili taarifa ya mwenendo wa zao la Chai kuanzia Mwaka 2022 hadi 2023 pamoja na kujadili utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa wadau.
Kuwasilisha taarifa ya mwenendo wa Tasnia ya Chai nchini ikiwa ni Pamoja na: –
Usajili wakulima wa zao la Chai,
Uhamasishaji maendeleo ya Tasnia ya Chai, ‘
Uendelezaji wa zao la Chai katika Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa,
Maendeleo ya mnada wa Chai wa kimtandao Dar Es Salaam,
Hali ya ulipaji wa madeni sugu ya wakulima wa Chai nchini,
Hali ya uendeshaji wa viwanda vya uchakataji wa chai
Upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za Chai (Miche bora, mbolea na viuagugu)
Kuwasilisha na kuthibitisha Mpango Mkakati wa Tasnia ya Chai (Tea Industry Strategic Plan) na mpango mkakati wa Taasisi ya Chai(Corporate Strategic Plan) ni mambo yatakayojadiliwa pia.
Hoja zingine ni uwasilishaji wa Taarifa ya Wadau wa Tasnia ya Chai na mapendekezo ya bei elekezi ya majani mabichi ya Chai kwa mwaka 2024
Aidha, katika mkutano huo, Bodi ya Chai Tanzania itatoa tuzo kwa wadau wa Maendeleo wenye mchango mkubwa katika Tasnia ya Chai Tanzania.