KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe Denis Londo imepokea na kujadili taarifa ya Mkoa wa Mwanza ya utekelezaji wa mpango wa bajeti fungu 81 kwa mwaka 2023/24 kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Februari 2024 na mapendekezo ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2024/25.
Kupitia kikao hicho kamati imeziagiza Halmashauri za Mkoa wa Mwanza ambazo bado hazijalipa madeni waliyokopa kupitia Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa kuhakikisha wanailipa na kusisitiza kuziita halmashauri ambazo bado hazijakamilisha urejeshwaji wa mikopo hiyo.
“ Kamati inatambua zipo Halmashauri ambazo bado hazijarejesha mikopo ambayo walikopa kupitia Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, hivyo ni wito wetu kwenu kuhakikisha mnarejesha mikopo hiyo na halmashauri ambazo bado tutaziita ili zitueleze kwanini hazijalipa mikopo hiyo,” Amesema Mwenyekiti wa Kamati, Mhe Londo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Dkt Festo Dugange, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Sospeter Mtwale, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla na wataalamu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI.