………………………
Na Ashrack Miraji Same
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango amezitaka mamlaka za uhifadhi wa misitu nchini kujipanua na kutoa elimu zaidi kwa wananchi namna ya kupanda miti ambayo inaendana na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Dkt. Mpango ametoa agizo hilo wilayani Same Mkoani Kilimanjaro katika maadhimisho ya siku ya misitu duniani pamoja na upandaji miti kitaifa maadhimisho ambayo yanafanyika kitaifa wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Amesema mwanzoni nchi ya Tanzania ilikuwa na vyanzo vingi sana vya maji lakini vimekuwa vikipungua Kutokana na uharibifu wa mazingira pamoja na uoteshaji miti ambayo ni adui kwenye vyanzo vya maji.
“Nakumbuka sana mwanzoni nchi hii ilikuwa na vyanzo vingi sana vya maji lakini vimekuwa vikipungua kila leo Kutokana na uharibifu wa mazingira pamoja na uoteshaji miti isiyorafiki kwenye vyanzo vya maji mfano wa miti ambayo ni adui mkubwa sana wa vyanzo vya maji ni mti aina ya mkaratusi mti huu umekuwa ukioteshwa kwenye vyanzo vya maji maeneo mengi Nchini na wananchi pasipo kujua athari yake hivyo ifike mahali sasa nyie wataalam mshuke vijijini kuwaelimisha wananchi aina za miti ambayo ni rafiki na vyanzo vya maji ili kuendelea kutunza vyanzo hivyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na hata kizazi cha baadae,”Amesema DKT.Mpango.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewataka wananchi kote nchini kutumia nishati mbadala ya gesi katika matumizi ya nyumbani kwa kupikia na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakichochea ukataji wa miti kiholela kwenye maeneo mbalimbali ya wananchi.
Kwa upande wake Waziri wa maliasili na Utalii Angellah Kairuki amesema miongoni mwa wilayani zinazokabiliwa na changamoto kubwa ya ukame Nchini ni pamoja na Wilaya ya Same kwani wananchi wake wamekuwa wakifanya shughuli ambazo zinakinzana na mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema kama Mkoa wamekwisha otesha zaidi ya miti milioni nane kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa huo.