*Yaridhishwa na namna Serikali inavyotenga Fedha miradi ya Nishati*
*Yataka Wizara kuongeza kasi kwenye utekelezaji wa bajeti 2023/2024*
*TANESCO Yatakiwa kuimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme*
*Wizara yaahidi kutekeleza maagizo ya Kamati*
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya wizara ya Nishati na kufikia lengo la utekelezaji kwa bajeti ya mwaka 2023/2024.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. David Mathayo, wakati kamati hiyo ilipopokea taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa Fedha wa 2023/2024, iliyowakutanisha pia na wakuu wa taasisi na idara zilizoko chini ya Wizara ya Nishati.
“Kipekee nimpongeze sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Biteko na wizara kwa ujumla kwa kutekeleza miradi kwa wakati na Serikali kwa kutenga Fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.” Alisema Mhe. Mathayo
Aidha Mhe. Mathayo alisema kuwa, licha ya Wizara kufanya vizuri kwenye utekelezaji wa miradi, ameiagiza TANESCO kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya umeme, kwani ndio muhimili wa uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kumekuwepo na mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya mwaka 2023/2024 ambapo mafanikio makubwa ikiwemo kuanza kwa uzalishaji wa umeme kiasi cha Megawati 235 Kwenye mradi wa Julius Nyerere na kuingizwa Kwenye Gridi ya Taifa, kukamilika kwa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyetezi I Extension kiasi cha Megawati 185 na kufanya jumla ya mitambo 4 kuwa inafua umeme kiasi cha Megawati 40 kila mmoja na kuingizwa Kwenye Gridi ya Taifa.
Aidha Mhe. Dkt. Biteko alisema kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa kwenye utekelezaji wa umeme vijijini ambapo jumla ya vijiji 11,837 sawa na asilimia 96.1 ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania bara vineunganishwa na umeme na kuongeza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua kupeleka umeme kwenye maeneo ya vitongoji.
Akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mkurugenzi wa Mipango na Sera kutoka Wizara ya Nishati Petro Lyatuu, alisema katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 utekelezaji wa miradi ya umeme imeimarika ikiwemo kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa uhakika na unaokidhi mahitaji ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii, ambapo hadi kufikia mwezi Februari 2024, uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa Kenya Gridi ya Taifa ulifikia jumla ya megawati 2,129.85.
Kwa upande wa uendeleaji miradi ya jotoardhi, Lyatuu alisema, katika kipindi cha mwezi julai 2023 hadi Februari 2024, Serikali kupitia TGDC iliendelea na ujenzi wa miundombinu na uchorongaji wa visima vya uhakiki kwa mradi wa Kiejombaka na Ngozi chini ya mshauri elekezi.
Kwa upande wa Sekta ya Mafuta, Lyatuu aliongeza kuwa sekta ya Mafuta chini ya Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja (PBPA) iliimarika ambapo ambapo kwa kipindi cha mwezi Julai 2023 hadi Februari 2024, akiba ya mafuta ilikuwa juu kwa siku 15, huku udhibiti na usimamizi wa shughuli za utafutaji wa Mafuta na gesi ukiendelea kupitia PURA na EWURA kuhakikisha mafanikio ya sekta hiyo chini ya maagizo ya Mhe. Rais ya kuhakikisha wananchi wananufaika na matunda ya uwekezaji kwenye maeneo yao.
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini waliwasilisha maoni mbalimbali ambapo Mbunge Ilemela Mhe. Angelina Mabula, Mhe. Jesca Kishoa Mbunge wa Viti Maalumu Iramba Mashariki na Mhe. Joseph Kasheku Msukuma wameipongeza Wizara kupitia taasisi zake kwa ufanisi wa utekelezaji wa miradi na kutaka wakandarasi wanaotekeleza miradi hususani ya umeme kuhakikisha wanafanyiwa upembuzi yakinifu kabla ya kupewa miradi.