Na Takdir Ali. Maelezo. 20.03.2024.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Habiba Hassan Omar amewataka Watoa huduma wa Hospitali za Serikali kuwa na kauli nzuri na matibabu bora ili kuweza kukabiliana na ushindani na Hospitali binafsi.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua mafunzo kwa watoa huduma wa Hospitali za Serikali huko katika Ukumbi wa Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Michenzani Mall Wilaya ya Mjini.
Amesema tokea Mfuko wa huduma za afya Zanzibar (ZHSF) kuanza kutoa huduma za Bima Oct, mwaka jana, idadi ya Wanachama wa Bima wanaokwenda katika Hospitali za Serikali ni ndogo ikilinganishwa na Hospitali binafsi.
Aidha amewataka Watoa huduma hao wa Hospitali za Serikali kuwahudumia kwa upole na unyenyekevu Wateja wao na sio kuwaengezea presha ili waweze kuachana na mitizamo ya kuwa huduma bora zinapatikana Hospitali binafsi pekee.
“Tunataka ushindani na hizi Hospitali binafsi, nendeni mukabadilishe mitazamo ya Watu,sisi tunataka huduma zote zitolewe sawa ibakie yeye Mwananchi kuenda Serikalini au binafsi.” alisema Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya.
Amefahamisha kuwa Serikali imejenga Hospitali kila Wilaya ili huduma ziweze kuboreka na kuridhisha kwa Wananchi wanaokwenda kupata matibabu.
“Hospitali za Wilaya tunaziona, Miondombinu ya Afya imeboreshwa na mambo mengine tele hivyo fufanye kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliowekwa na Serikali.” Alisema Katibu Mkuu hiyo.
Mapema akiwasilisha mada katika Mafunzo hayo Meneja masoko na kukuza Biashara kutoka Banki ya Watu wa Zanzibar Pbz Seif Suleiman Mohammed amewataka kutumia lugha nzuri kwa Wateja wao ili kuondosha migogoro baina ya Watendaji na Watoa huduma.
Aidha amewataka kuwasililiza wateja wao wanapokwenda na kuomba radhi kwa pale wanapokosea ili kutengeneza mahusiano mema baina ya Wananchi na watoa huduma hao.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kutoa huduma bora kwa wananchi sambamba na kuomba mafunzo yawe endelevu ili yazidi kuwajengea uwezo na kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo ya ZHSF kutoa huduma bora kwa wote.
Hata hivyo Washiriki hao wameahidi kutoa lunga nzuri kwa wateja wao wanaofika katika hospitali ili kunusuru athari zinazoweza kujitokeza.