Mkurugenzi Mtendaji wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Bill Kiwia (kushoto) na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Bw. Juma Mohamed (kulia) wakitia saini ya hati ya makubaliano katika hafla iliyofanyika leo Machi 18, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Bill Kiwia (kushoto) , Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Bw. Juma Mohamed (kulia) wakishika hati ya makubaliano baada ya kusaini leo Machi 18, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Bill Kiwia akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuingia makubaliano na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) katika utekelezaji wa majukumu yao.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesaini hati ya makubaliano na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kwa ajili ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuandaa mafunzo ya kuongeza ujuzi katika sekta ya utalii pamoja na kutafuta fursa za ajira kwa wanufaika ili kuwawezesha kurejesha.
Akizungumza leo Machi 18, 2024 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini wa hati ya makubaliano kati ya HESLB na ZEEA, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dkt. Bill Kiwia, amesema kuwa ushirikiano huo umelenga kuongeza kasi ya urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wajasiriamali walionufaika na mikopo ya elimu ya juu.
Dkt. Kiwia amesema kuwa ushirikiano utaongeza ufanisi kwa taasisi zote mbili
HESLB na ZEEA kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
“Kupitia makubaliano haya tunatarajia wanufaika ambao wako katika sekta ya isiyo rasmi watajitokeza na kuanza kurejesha mikopo yao” amesema Dkt. Kiwia.
Amesema kuwa wanatarajia kuwa na ongezeko la wanafunzi wahitaji kunufaika na fedha zinazorejeshwa na kuufanya mfuko kugharimia wanafunzi kwa stahimilivu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Bw. Juma Mohamed, amesema kuwa ushirikiano huo unakwenda kuleta tija kwa wanufaika kuanza kurejesha mikopo ambao hawapo katika sekta isiyokuwa rasmi.
Bw. Mohamed amesema kuwa ushirikiano huo na HESLB watapata taarifa za wanufaika pamoja na kuwawezesha kuingia katika mfumo wa sekta ya ajira.
HESLB ina majukumu mawili; utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu, tangu kuanzishwa kwake watanzania 754, 000 wamenufaika kwa kutumia shilingi trilioni 7.2 kwa ajili ya kugharimia masomo yao ya elimu ya juu.
Kuanzia mwaka 2007 mpaka sasa kiasi cha shilingi trilioni 2.1 kimekusanywa kutoka kwa wanufaika zaidi ya 448, 882, huku wanufaika 222, 532 bado hawajaanza kurejesha mikopo yao.