……………….
Na Sixmund Begashe
Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW), umezidi kuwa neema kwa uhifadhi wa Ikolojia pamoja Utalii katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kutokana na Maboresho ya mito uliofanywa Wilaya ya Mbarali yamesaidia kutiririsha maji kwenye Mto Mkuu wa Ruaha na kufanya Mto huo kuwa na maji mengi ambayo yamekuwa neema kwa wanyama na mimea.
Akizungumzia Mto huo unaopita kwenye Hifadhi ya pili kwa ukubwa Tanzania, Mkuu wa Hifadhi hiyo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Godwell Meing’ataki amesema Mto huo umekuwa ukikumbwa na ukame kwa zaidi ya miezi mitano na kusababisha shida kwa wanyama na viumbe vingine vinavyotegemea mto huo.
“Kwa sasa Mto umejaa maji, tunaona namna wanyama wanavyo nufaika, hii ni kutoka na kazi kubwa inayofanywa na Mradi wetu wa REGROW ya kuhakikisha maji kwenye Mto huu hayakauki, yanatiririka mwaka mzima hali itakayo changia upatikanaji wa maji kwenye Bwawa la kufulia umeme la Mwl Nyerere.” Amesema Meing’ataki
Meing’ataki ametoa wito kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji Mto Ruaha Mkuu, na kuwataka wale wenye tabia ya kuzuia maji kutokana na shughuli za kijamii wasifumbiwe macho bali wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Aidha Meng’ataki amefafanua kuwa, matokeo chanya ya utekelezaji wa mradi wa REGROW yanayoonekana kwenye Mto Mkuu Ruaha, ni mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan ambaye inaelekea kutimiza miaka mitatu madarakani.
Mradi wa REGROW unaotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia umeendelea kuwa neema kubwa kwa usalama wa chakula, maji, upatikanaji wa umeme wa uhakika, uhifadhi endelevu wa Maliasili pamoja na kukuza Utalii nchini.