Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Dk Batilda Burian, amewahimiza watumishi wa umma kushiriki matendo ya huruma hasa kipindi hiki cha mfungo wa Kwaresma na Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mhe Dk Batilda ameyasema hayo leo ofisini kwake, wakati akizungumza kwenye hafla ya kumuapisha Mkuu wa Wilaya ya Mkinga aliyeteuliwa Machi 9, 2024, Mhe Kanali Evans Mtambi.
Amesema matendo ya huruma yanayojumuisha kuwasaidia watu wenye uhitaji ni sehemu ya sadaka inayojibu maombi ya mtoaji, lakini pia ni sehemu ya misingi ya utumishi wa umma.
‘’Msisubiri hadi muombwe ndipo muende mkafanye matendo ya huruma kwa wahitaji, nendeni kila mnapoona kuna uhitaji, na kupitia sadaka hiyo maombi yetu yatajibiwa na kukuokoa kwenye shida,’’ anasema.
Mhe Dk Burian amefafanua kuwa, kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum hasa wasiojiweza, kunaashiria pia utayari wa watumishi wa umma kuwa karibu na wananchi wanaowatumikia.