Ndugu Selemani Sankwa – Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga.
…………………
Na: Mwandishi wetu, Tanga.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga kimedhamiria kushinda viti vyote vinne vya udiwani kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika Machi 20 mwaka huu. Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga Ndugu Selemani Sankwa alipokuwa akitoa mwelekeo wa kampeni kwenye kata nne ndani ya mkoa wa Tanga ambapo uchaguzi utafanyika.
“CCM Mkoa wa Tanga tuna uhakika wa kushinda kata zote nne ambazo ni Mkuzi wilayani Muheza, Boma, Mtimbwani na Mayomboni zilizopo Wilaya ya Mkinga. Ninaposema tuna uhakika wa ushindi si kwamba nabahatisha au najifariji bali ushindi wetu unatokana na utekelezaji wa Ilani ya CCM uliofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika kata hizo tumeshuhudia ujenzi wa miradi ya Elimu, Afya, Umeme, Maji, Barabara na mingineyo.” amesema Sankwa
Mtendaji huyo Mkuu wa Chama Mkoa wa Tanga aliendelea kusisitiza kuwa “Tunajivunia kazi kubwa iliyofanywa na Viongozi wa Chama Wilaya na Mkoa chini ya Ndugu Rajabu Abdallah (MNEC) ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga ya kuisimamia Serikali katika Miradi ya Maendeleo ambayo ni chachu ya kuchaguliwa kwetu.”
Vilevile, Sankwa amesema CCM inaamini katika kuwatumika wananchi kikamilifu kama siri ya ushindi wake, na ndiyo maana viongozi wa chama na serikali wamejitahidi sana kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Hatua hatua nyingine, Sankwa amesema Chama kimefanikiwa kuendesha vyema uchaguzi wa kura za maoni ambapo wagombea wamepatikana huku umoja na mshikamano wa Wanachama ukibaki imara bila makundi ya aina yeyote. “Niwasihi Wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya Uchaguzi ili kutumia haki yao ya kuchagua Viongozi bora wanaotokana na CCM.” amesema Sankwa.
Februari 15, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza uchaguzi mdogo wa Udiwani katika kata 23 za Tanzania Bara ambapo Uchaguzi utafanyika Machi 20. Kata nne ndani ya Mkoa wa Tanga zitafanya Uchaguzi mdogo huku CCM ikijinadi kushinda kata zote kwa ushindi wa kishindo.