Na Mwandishi wetu, Mirerani
MUSTAKABALI wa vitambulisho vya kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, bado haujafikiwa muafaka baada ya kuongezwa muda wa majadiliano.
Vitambulisho hivyo vitakavyomilikiwa na eneo tengefu la Mirerani, vilipendekezwa kulipiwa shilingi elfu 10 kwa kila kitambulisho na kutumika kwa muda wa mwaka mmoja.
Ofisa madini mkazi (RMO) wa Mirerani, Chacha Marwa, akizungumza na wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite, amesema watakutana na Mwenyekiti wa kamati ya ukuta ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro ili kujadili hilo.
Awali, RMO Chacha amesema sheria ya uanzishwaji eneo tengefu la Mirerani, kupitia kanuni ya 15 inaelekeza kutumika kwa vitambulisho pindi mtu anapotaka kuingia ndani ya eneo hilo.
Amesema endapo mgeni anaingia kwa siku moja katika eneo tengefu la Mirerani anapaswa kupatiwa kitambulisho cha ugeni ambacho ni tofauti na vitambulisho vingine.
Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani (OCS) Mrakibu wa polisi (SP) Dominick Fwaja amesema faida za vitambulisho hivyo ni kuwakamata kiurahisi watu watakaofanya uhalifu ndani ya ukuta huo.
“Vitambulisho hivyo vitaunganishwa kwenye mfumo wa ulinzi na usalama wa ukuta, ambao utaweza kubaini mahali mhalifu alipotorokea popote baada ya kufanya uhalifu,” amesema OCS Fwaja.
Hata hivyo, mmoja kati ya wachimbaji madini ya Tanzanite, Samwel Rugemalira ametoa tahadhari juu ya zoezi hilo kwani suala la vitambulisho vya Taifa lilishawahi kuondoka na Mawaziri watatu wa Mambo ya Ndani.
Mchimbaji mwingine Hossea Palangyo (Shilingi) amesema vitambulisho hivyo vitawapa mzigo mkubwa wachimbaji hao kwani kumlipia kila mfanyakazi shilingi elfu 10 ni gharama kubwa.
Mwenyekiti wa wanaApolo Idd Malamsha amesema haoni umuhimu wa vitambulisho vipya kwani wachimbaji wana vitambulisho vya Taifa ambavyo bado wanavitumia.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani, Jumanne Nahe akifunga kikao hicho amesema watateua wawakilishi wao ili wakutane na kamati ya ukuta na kujadili mustakabali wa vitambulisho hivyo.
Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani, Rachel Njau amesema wameandaa mkutano huo kwa lengo la kukutanisha viongozi wa serikali na wachimbaji ili kujadili mustakabali wa vitambulisho hivyo.