Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wabobezi kutoka nchini Sudan imeanza kambi maalumu ya upasuaji rekebishi wa macho ambao unahusisha watu wenye uvimbe nje ya jicho, makengeza kwa watu wazima, majeraha yatokanayo na ajali au makovu ya muda mrefu ya macho, wanaotoka machozi kwa muda mrefu kutokana na kuziba kwa njia za machozi.
Pia kambi hiyo imeshirikisha madaktari wazawa kutoka Muhimbili Upanga, Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi, Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mtwara Ligula, Hospitali ya Kanda Mbeya na St. Benedict Lindi.
Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Macho wa Muhimbili Mloganzila Catherine Makunja kabla ya kuanza kwa upasuaji huo, jana Machi 11, 2024 jopo la wataalamu liliwaona na kuwafanyia uchunguzi wa awali wagonjwa wenye matatizo hayo ambao wamejitokeza.
Dkt. Makunja amesema kufuatia kuanza kwa kambi hiyo, leo wamefanyia upasuaji wa macho wagonjwa wenye changamoto ya kufunga kwa vifuniko vya macho na zoezi hilo limeenda vizuri bila changamoto zozote na baadhi yao wameruhusiwa kurudi nyumbani .
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imekuwa ikitoa matibabu ya ubingwa bobezi kwa matibabu ambayo hayapatikani hapa nchini na hivyo kuwapunguzia wananchi adha ya kwenda nje ya nchi kutafuta huduma hizo, miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na huduma ya kupunguza uzito kwa puto maalum (intragastic balloon) , upasuaji wa kupunguza uzito (bariatric surgery), upandikizaji wa figo kwa kuvuna figo kwa kutumia matundu madogo na kutoa uvimbe kwenye ubongo kwa kutumia tundu dogo.