ZAIDI ya nyumba 500 zimebomoka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika kata ya Mbondo na Kilimarondo wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama pamoja na Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Nachingwea, Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa nyumba zaidi ya 500 zimetoka hivyo kamati ya Maafa inafanya tathimini ya Maafa yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kuwapa pole wahanga hao.
Moyo alisema kuwa Kata ya Kilimarondo jumla nyumba 326 ambapo nyumba 223 zianguka kabisa na nyumba 103 zimewekwa nyumba kutokana na mvua. Katika nyumba hizo, Kijiji cha Kilamarondo ziko nyumba 108, Kijiji cha Nanjii ziko nyumba 83 na kijiji cha Namatunu ziko nyumba 135
Katika kata ya Mbondo jumla ya kaya 290 zimebomolewa nyumba zao na kusababisha jumla ya wakazi 836 kukosa makazi na kupoteza mali zao nyingi. Maafa hayo yametokea katika vijiji vya kata hiyo kama ifuatavyo katika kijiji cha Chimbendenga kaya 67, Mbondo kaya 149, Nakalonji kaya 36 na kijiji cha Naimba kaya 38
Moyo alisema kuwa kwa upande wa kilimo mashamba mengi yameathiriwa kwa kujaa maji na hali hiyo imepelekea mazao kudumaa na kubadili rangi kabisa Kitu kitakachosababisha uzalishaji kupungua kwa kasi kubwa kwa mwaka huu (2024) na mazao hayo ni Mahindi, mihogo, mtama na kunde.
Mvua imeharibu takribani heka 2245 kwa kata ya Kilimarondo. Pia, miundombinu imeharibiwa, barabara zinazounganisha kijiji na kijiji hazipitiki na kufanya baadhi ya shughuli za uzalishaji kusiamama au kupungua.
Moyo alimalizia kwa kuwataka wananchi kujenga nyumba imara na za kisasa ambazo zitahimili mvua kubwa za Masika na kusema kuwa kwa sasa kata hizo hazina njaa ila kwa baadae inaweza kutokea njaa kutokana mvua kuharibu mazao ya wakulima.