KATIKA kuunga mkono agenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuinua wanawake, Benki ya Mwalimu Commercial imezindua akaunti ya tunu kwa ajili ya wanawake na vijana.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam na Mkuu wa Kitengo cha ukuzaji biashara na masomo kutoka Benki hiyo, Leticia Ndongole katika halfa ya kusherekekea siku ya wanawake Dunia iliyowakutanisha jukwaa la viongozi wanawake wa Mashirika ya umma.
Amesema kwa miaka sita, ambayo wamekuwa katika soko wameweza kutoa bidhaa hiyo kwa wanawake .
“Kwa mwaka 2024 tumeona tuweze kushirikiana na Taasisi za umma sambamba na kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ajenda ya kuinua wanawake,”amesema Leticia.
Amesema wamekuwa wakitoa huduma kwa walimu Tanzania nzima pamoja na wanawake waliopo katika ngazi zote katika jamii.
Aidha aliongeza kuwa katika kuazimisha siku ya wanawake Dunia Machi 8 wameona ni vema kushirikina na wanawake katika kuzindua bidhaa hiyo .
Vilevile amesema wanawake wamekuwa wakisukumwa na ajenda moja ya kumuwezesha ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi Kwa Taifa .
“Tumeona ni vema kuzindua bidhaa hii ya tunu tunaamini Kwa ushiriki wa wakuu wa Taasisi za umma tutaweza kuwafikia wanawake wengi katika ngazi zote.
“Asilimia kubwa ya wanawake ndio wamekuwa wakikuza uchumi hasa katika sekta binafsi…Kama Mwalimu commercial Bank tumeona tunaowajibu wa kuhakikisha kwamba tunaweza kuwasaidia wakinamama katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuwaingiaza katika sekta ya fedha Kwa kuwapatia elimu katika upande wa kuwekeza na hatimaye kukuza biashara yao,”amesema Leticia.