*Asema mfano mzuri ni kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ameyasema hayo leo Machi 08, 2024 wakati akitoa hotuba ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani katika Mkoa huo yaliyofanyika katika Uwanja wa Mji Mwema Wilaya ya Kigamboni.
RC Chalamila amesema tunapoadhimisha Siku ya tarehe 08 machi kila mwaka ni vema kutafakari nafasi ya mwanamke katika familia, Jamii na Taifa kwa Ujumla ” Kila mwanamke atambue ana nafasi kubwa na muhimu Katika Taifa mfano mzuri ni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni mwanamke hodari na mahiri kila mmoja anaona uongozi wake namna Taifa linavyo Songa mbele katika nyanja mbalimbali chini ya uongozi wake” Alisema RC Chalamila
Aidha amesema mwanamke ni Mwalimu, ni Daktari, ni Mchumi, ni Afisa Mipango, ni Afisa Uhusiano ni mbunifu ni mbeba maono na mengine mengi yanayofanana na hayo hivyo siku ya leo ni muhimu kutafakari hayo yote kwa masilahi mapana ya ustawi wa jamii.
Sambamba na hilo RC Chalamila amesema wanawake licha ya kuwa na mchango mkubwa katika makuzi ya uchumi na ustawi wa Jamii na Taifa kwa ujumla amekuwa akipitia makwazo na manyanyaso mengi katika jamii tena yanayosababishwa na wanaume au mifumo kandamizi katika jamii hivi kupitia maadhimisho haya ya leo ni vema wanawake kwa umoja wao kujiimarisha na kuikataa mifumo hiyo kandamizi.
Ifahamike kuwa kila ifikapo machi 8, kila mwaka Duniani kote wanawake huadhimisha maadhimisho hayo ambayo huambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiliamali wazawa, katika Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amezindua pia Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika Mkoa huo.