Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB), Mhandisi Rhoben Nkori amewakemea baadhi ya Makandarasi wanaofanya kazi kwa mazoea kuacha tabia hiyo huku akieleza Bodi haitasita kuwafutia usajili wa kampuni zao.
Alisema kwa sasa Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa miradi mingi kutekelezwa na Makandarasi wazawa lakini kuna baadhi wamekuwa wakitumia fursa hiyo kuijengea taswira mbaya tasnia hiyo kwa kufanya kazi bila kuzingatia weledi.
Hayo aliyasema leo Dar es Salaam wakati akiongea na Makandarasi zaidi ya 170 waliokuwa wakishiriki mafunzo ya siku tatu yaliyokuwa yanalenga kuwajengea uwezo na ujuzi wa namna ya kuandaa zabuni, kujaza mikataba, utekelezaji wa mikataba ya ujenzi, elimu ya kodi na namna ya kuzisimamia na kuboresha kazi zao.
“Kwa Makandarasi ambao wataonekana kuichafua tasnia hii kwa kufanya kazi kwa mazoea tunaomba ushirikiano wenu tuweze kuwaondoa kwenye usajili wabakie wale wenye sifa zinazotakiwa na si vinginevyo,”
” Matukio ya ovyo yanapotokea yanachafua tasnia na yanawaharibia nyie wote,wako Makandarasi wengi wazuri lakini kuendelea kuwapuuza wanaofanya matukio ya ovyo hawatatujengea heshima, tunaomba ushirikiano mkiwaona basi wanafanya hivyo msikae kimya,” alisema Nkori.
Katika maelezo yake Mhandisi Nkori alisema Makandarasi hao wasipotoa taarifa kwa wale watakaoonekana wanafanya kazi kwa mazoea basi watakuwa wanaunga mkono maovu hayo hivyo watakuwa wamejiweka katika mazingira magumu.
“Mafunzo haya lazima muyaunganishe na kazi mnazofanya kama mnahisi mnachofundishwa hamuwezi kukihusianisha na shughuli mnazofanya mtakuwa mnajifedhehesha wenyewe, Bodi na Serikali inatumia gharama kubwa kuandaa mafunzo,” alisema Nkori.
Alisema Serikali imejikita kutengeneza sera na mifumo rafiki ili Makandarasi wa ndani wafanye kazi kwa uhuru kwa kuzingatia weledi,sheria na taratibu zilizopo kama unaenda kukopa basi kopa kiasi kulingana na thamani ya mradi anaotekeleza.
“Usiende kutekeleza mradi kwa kutegemea kukopa kwenye kikoba,sheria zipo lakini tunaomba Makandarasi fanyeni kazi kwa weledi kinyume na hapo bodi haitasita kumchukulia hatua mkandarasi yeyote atakayebainika kufanya kazi kwa mazoea kwa kufutwa kwenye usajili,” alisema
Adhabu kwa watakaobainika kuichafua tasnia
Alisema, Mkandarasi akifutiwa usajili hatakiwi kusajili Kampuni hiyo ndani ya muda wa miaka mitatu na mmiliki wa kampuni husika hawataruhusiwa kujiunga na kampuni nyingine ya ukandarasi hadi miaka miwili ipite.
“Ukiwa unafanya kazi kwenye kampuni fulani itendee haki lakini ikibainika ikafutwa kutokana na makosa ya kutokuzingatia sheria na taratibu zilizopo hamruhusiwi kusajili kampuni nyingine na kwa jina lingine hadi miaka mitatu ipite,” alisema Msajili
Alisema wamiliki hawaruhusiwi kwenda kushika nafasi ya Mkurugenzi kwenye kampuni yeyote ile hadi kipindi cha miaka miwili ya kutumikia adhabu ya kufutwa iishe.
“Pia naowaomba wamiliki wa makampuni heshimuni taaluma sitegemei Mhadisi afanye shughuli za fedha ni lazima katika nafasi hiyo apatikane mtaalamu husika ili kuleta tija katika kazi,”
Alisema baada ya kupata mafunzo hayo anategemea wabadilike na wafanye kazi kwa weledi ili kuijengea taswira nzuri kwa jamii hasa kwenye miradi wanayopewa kuisimamia.