Na Sophia Kingimali
Naibu waziri mkuu na Waziri wa nishati Doto Biteko ametoa rai kwa wananchi kutunza mazingira na vyazo vya maji ili kuhakikisha miundombinu ya uzalishaji wa umeme inatunzwa ili kuepuka adha ya ukosefu wa umeme nchini.
Hayo ameyasema leo March 7,2024 jijini Dar es salaam wakati wa Hafla ya ugawaji vitendea kazi kwa wanawake wajasiliamali na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kugawa majiko ya gesi ya Oryx kwa wajasiliali wa wilaya ya Temeke iliyofanyika katika viwanja vya Zakhiem
Amesema changamoto ya umeme imefikia mwisho kwani kwani kilichobakia ni kukamilisha miundombinu ya kusafirishia umeme kutoka bwana la kuzalishia umeme la Mwalimu Nyerere na kwenda kwenye vyanzo vingine vya kuzalishia umeme.
“Tunaenda kumaliza changamoto ya umeme nitoe rai kwa wananchi kulinda bwawa hilo ambalo ndio tegemeo letu kubwa kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika shughuli za binadamu zisifanywe pale ili tusije tukarudi kwenye janga hili la ukosefu wa umeme”,amesema.
Akizungumzia matumizi ya nishati mbadala amesema agenda hiyo si ya serikali pekee hivyo taasisi zote zinapaswa kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Amesema serikali itaendelea kuhasisha matumizi ya nishati safi hasa kwa kuwawezesha wanawake kutumia nishati safi ya kupikia kwani waathirika wakubwa katika matumizi ya nishati ni wao.
“Tutaendelea kumthamini mwanamke wa tanzania kwa kumuwezesha kupata nishati safi ya kupikia kwani kinara wa matumizi ya nishati mbadala ni Rais wetu Dtk Samia Suluhu Hassan na amedhamilia kwa dhati kumuinua mwanamke na kumuepusha na madhara yatokanayo na matumizi ya nishati itokanayo na mkaa na kuni”Amesema
Sambamba na hayo ametoa rai kwa magereza yote nchini,Shule na Taasisi zote kubadilisha mifumo yake ya kupikia inayotumia kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi.
Aidha ameiagiza mamlaka ya misitu kulinda uvunaji wa halamu wa misitu ili kuendelea kutunza mazingira.
Kwa upande wake naibu waziri wa nishati Judith Kapinga amesema wameandaa kongamano kwa ajili ya kusheherekea siku ya mwanamke lakini pia kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala hivyo ametoa rai kwa wanawake wengi kujitokeza.
Amesema Takribani asilimia 35 ya wanawake bado wanatumia mkaa hivyo wataendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi lakini pia kuendelea kugawa vitendea kazi kwani kwa awamu hii watagawa vitendea kazi elfu 10 kwa wilaya zote na wataendelea kufanya hivyo kila wanavyopata rasilimali hiyo.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa kampuni nyingine za nishati kuiga mfano wa Oryx kwa kuwasaidia wananchi kupata nishati hiyo mbadala.
Kwa niaba ya watoa huduma wa nishati mbadala Mkurugenzi Mtendaji wa ORYX Tanzani Araman Benoit mesema matumizi ya gesi yanasaidia kutunza mazingira kwa kutokukata miti lakini pia kulinda afya ya watumiji.
Amesema uvutaji wa hewa chafu inayotokana na matumizi ya kuni na mkaa inamsabibishia mtumiaji(mwanamke) kuwa na afya mbaya.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Temeke Zena Mgaya amesema wakinamama wanaiona faida ya kuwa na kiongozi mwanamke kwani amekuwa akionyesha juhudi mbalimbali za kuwasaidia wanawake hivyo wanamuahidi Rais samia kumpa kura nyingi ili aendelee kuwasaidia wanawake nchi nzima kama anavyofanya sasa.