Na Sixmund Begashe
Wataalam kutoka Bank ya Dunia wanaendesha semina kwa Wataalam wanao simamia utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) juu ya mfumo wa upokeaji na kushughulikia malalamiko pale yanapotokea wakati wa utekelezaji wa mradi.
Akifungua Mafunzo hayo Mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo Dkt. Edward Kohi ameipongeza Banki ya Dunia kwa kuandaa Mafunzo hayo ambayo yataimarisha zoezi zima la upokeaji wa malalamiko na namna ya kuyashughulikia kwa wakati ili malengo ya mradi yafikiwe kwa wakati.
Dkt. Kohi ameongeza kuwa mfumo huo wa REGROW wa kupokea malalamiko ni muhimu kwakuwa unatoa nafasi kwa wananchi na wadau mbalimbali kutoa malalamiko au maoni yenye nia ya kuboresha zoezi zima la utekelezaji wa mradi kwa njia shirikishi.
Aidha ametoa wito kwa washiriki kuzingatia Mafunzo hayo ili kupata uelewa mpana wa kughulikia malalamiko si kwa mradi tu wa REGROW bali kwenye kazi za kilasiku za Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wakizungumzia mafunzo hayo ya siku mbili, Maafisa Wandamizi wa Maendeleo ya Jamii Banki ya Dunia, Bi. Roselyn Kaihula na Bi. Annette Omolo, wamesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalam wanotekelezaji mradi wa REGROW, namna ya kushughulikia malalamiko na changamoto mbalimbali kwa ufanisi zaidi hali itakayo pelekea zaidi kufikiwa kwa malengo kusudiwa ya mdari huo.