Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)Bernard Kongo akizungumza katika kikao kazi cha Ofisi ya Msajili wa hazina, Jukwaa la wahariri TEF na Mfuko huo kilichofanyika kwenye chuo cha utalii Posta jijini Dar es salaam Machi 7, 2024.
Thobias Makoba. mkuu wa Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina akizungumza na wahariri kabla ya Mkurugenzi wa NHIF Bw. Benard Konga kuwasilisha mada katika kikao hicho.
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kusudi akitoa maelezo kwa washiriki wa Kikaokazi hicho cha Wahariri kabla ya kuanza rasmi.
………………….
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepiga hatua kubwa sana kwenye kugharamia huduma za kibingwa bobezi za magonjwa ya Figo,Moyo na Saratani ikiwemo uboershaji wa kitita.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF Bw.Bernard Konga wakati akizungumzia mafanikio ya mfuko huo kwa miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kikao kazi kati ya Ofisi ya Msajili wa hazina,Jukwaa la wahariri (TEF) na Shirika hilo kilichofanyika leo Machi 7, 2024 Chuo cha Utalii Posta Jijini Dar es Salaam.
Amesema kwa mwaka 2022,2023 jumla ya bilioni 32.46 zilitumika kulipia huduma za saratani katika Hospital ya Osheni road, Bugando na KCMC ambapo zamani watu walikuwa wanaenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata huduma hiyo lakini kwa sasa huduma inapatika nchini.
Amesema huduma za Figo kwa mwaka 2022,2023 wamechangia bilioni 35.4 ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo walichangia bilioni 11.
“Huduma za Figo zinagharama kubwa na kama nchi tuna wagonjwa wa aina hiyo kati yao asilimia 75 ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)”, amesema Konga
Ameeleza kuwa magonjwa hayo siyo ya kurithi hivyo ni vyema wananchi wakachukua tahadhari dhidi ya magonjwa hayo kwani matibabu yake yanagharama kubwa.
“Wananchi wasipochukua tahadhari ya magonjwa hayo Fedha nyingi tunazozitenga kwenye Sekta ya afya zitakuwa zinaenda kwenye matibabu ya magonjwa hayo, pia tunawakumbusha watanzania kuingia kwenye mfumo wa bima kwa ajili ya kupata unafuu wa gharama za matibabu “, ameeleza Konga
Aidha, ameeleza kuwa Soko la Bima ya Afya nchini lina asilimia 15 ambapo asilimia 8 ni NHIF asilimia 6 ni CHF na asilimia Moja ni bima binafsi hivyo bado kuna asilimia 85 za kuirejesha kwenye mfumo wa bima ya afya nchini.
Katika asilimia 85 asilimia 26 ni kaya masikini kama nchi bado tuna nafasi kubwa yakuendelea mbele kwenye mfumo wa bima, pia kwa kipindi hiki wameweza kusaidia wanachama milioni 4.9 ambao wanawahudumia kama Mfuko kutoka Kwenye makundi mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma, taasisi na mwanachama mmoja mmoja.
Akizungumza kuhusu usajili wa vituo Bw.Konga amesema wamesajili vituo ambavyo wanafanya navyo kazi na hadi sasa wana vituo takribani 9186 vya Serikali 6800 binafsi na 1700 na mashirika ya dini 829.
Amesema mwaka 2016 nchi ilikuwa na na mashine za CT Scan 5 lakini kwa sasa zipo 50 na kwamba ni mafanikio makubwa yanayoendelea chini ya Serikali ya awamu ya sita.
Akizungumzia ongezeko la wanachama Konga amesema wamefanikiwa kuongeza wanachama katika mfuko huo kwani ulipoanzishwa mwaka 2001/2002 walikua na wanachama 164.708 huku wanufaika wakiwa laki 691.773 ambapo mpaka kufikia 2023/2024 wameongezeka wanachama na kufikia 1.246.046 huku wanufaikia wakifikia milioni 4,987,292 ambalo ni ongezeko kubwa kwa muda mfupi.